Jun 23, 2019 17:28 UTC
  • Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-16

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 16 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia umuhimu wa uhuru wa kijamii na kisiasa kwa mtazamo wa Imam Khomeini ambapo tulisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inatakiwa kutoa uhuru kamili kwa wakosoaji na wapinzani wa serikali, leo pia tutaendelea kuzungunzia suala hilo, karibuni.

Ndugu wasikilizaji akijibu swali la wale waliotaka kujua kiwango cha uhuru wa kidini wa jamii ya wachache katika kutekeleza wajibu na masuala yao ya kidini katika utawala wa Jamhuri ya Kiislamu, Imamu Khomeini (MA) aliweka wazi kwamba, katika utekelezaji wa majukumu yake ya kidini, si tu kwamba jamii ya wachache ina uhuru wa kutosha wa kutekeleza majukumu hayo, bali ni jukumu la serikali ya Kiislamu kutetea na kulinda kikamilifu uhuru huo. Imam alisema: “Jamii zote za kidini za walio wachache katika dola la Kiislamu zinaweza kutekeleza ibada zao kwa uhuru kamili na serikali inawajibika kulinda haki zao kwa njia bora zaidi.” Hotuba ya tarehe 17/8/1357.

 

******

Sambamba na kutenganisha idolojia ya Uzayuni na dini ya Uyahudu, aliwataja Mayahudi wa Iran kuwa raia wenye haki kamili chini ya utawala wa Kiislamu na wanaopasa kustafidi na ustawi wa nchi hii. Katika uwanja huo alisema: “Mayahudi wanaoishi Iran, ni watu ambao hawapaswi kufanyiwa mabaya, bali wao ni watu walio chini ya hifadhi ya Kiislamu na Waislamu……Inshallah iwapo serikali ya uadilifu itaasisiwa, Mayahudi wote ambao milki zao zipo nchini hapa wataitwa wote waweze kurudi nchini kwao na serikali ya Kiislamu itaamiliana nao kwa njia bora zaidi.” Hotuba ya tarehe 1/10/1357.

Mayahudi ambao wanapinga Uzayuni

 

Mtukufu huyo alitenganisha hali ya Uzayuni na Wazayuni mbali na Mayahudi kwa kusema: “Uhusiano wowote na utawala haramu wa Israel utakatwa, lakini Mayahudi nchini Iran wataishi kwa uhuru mkubwa zaidi kuliko kipindi cha utawala wa Shah iwapo watabakia nchini hapa. Hii ni kwa kuwa dini ya Uislamu inaheshimu dini zote.” Hotuba ya tarehe 24/10/1357.

******

Aina nyingine ya uhuru wa jamii za wachache nchini Iran ni kuhusiana na Waislamu wa Kisuni. Kwa kuzingatia kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yalisimamia juu ya idolojia ya Kishia, na katika kipindi hicho kulikuwa na baadhi ya wasomi wa Kisuni waliowatuhumu Waislamu wa Shia kuwa sio Waislamu na hata kufikia kuwaita kuwa ni makafiri, misimamo ya kisiasa ya Imam Khomeini (MA) kama marjaa mkubwa wa Kishia na pia kama kiongozi mkuu wa mfumo wa Kiislamu ambao ulisimama juu ya idiolojia ya Shia, ilikuwa ikichukuliwa kuwa muhimu na yenye kuzingatiwa sana. Watu wengi kipindi kile walikuwa wakitaraji kwamba baada ya viongozi wa Kishia kutwaa madaraka ya nchi, wangetumia fursa hiyo kwa ajili ya kukabiliana na Waislamu wenzao wa Kisuni sambamba na kupanua wigo wa Ushia. Hata hivyo Imam Khomeini kwa kutumia weledi usio na mfano, aliwataja Waislamu wote wa Shia na Suni kuwa ndugu wamoja katika dini na kwamba tofauti zao zilichochewa tu na maadui wa Uislamu. Katika uwanja huo mtukufu huyo alisema: “Sisi tunatangaza udugu wetu kwa ndugu zetu wa Suni.

Adui halisi wa umma wa Kiislamu ni utawala haramu wa Israel

 

Maadui wa Uislamu ndio wanataka kutuchonganisha na ndugu zetu hao.” Akizungumzia umuhimu wa umoja wa Waislamu kuwa unaoweza kusambaratisha njama za maadui na kwamba umoja kati ya Mashia na Masuni ni suala la wajibu alisema: “Lau kama Waislamu wangekuwa na umoja, basi maajnabi wasingeweza kutudhibiti. Tofauti hizi ambazo ziliibuka tangu mwanzo kupitia watu majahili, hii leo pia zimeendelea kutukabili. Ni wajibu kwa Waislamu wote kuwa kitu kimoja.” Hotuba ya tarehe 17/11/1357.

 

******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu 16 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia kiini na kichochezi cha Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya usimamizi wa Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Uhuru wa kuchagua ni moja ya masuala muhimu katika ushiriki wa kisiasa na moja ya mihimili mikuu ya mfumo wa kidemokrasia. Akthari ya wanafikra wa Kimagharibi wamelitaja suala la uhuru wa kuchagua kuwa lenye umuhimu mkubwa ambalo linatoa mwanga wa demokrasia kwa kila nchi. Kwa ibara nyingine ni kwamba katika mtazamo wa wanafikra wa Magharibi utambulisho unaoweza kutumika katika kuainisha mfumo wa kidemokrasia mbali na mfumo usio wa kidemokrasia, ni uchaguzi. Kwa kutilia maanani kwamba katika jamii viongozi wanatakiwa kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi huru na wa haki, mfumo huo ndio hupewa sifa ya demokrasia. Imam Khomeini kwa kuzingatia umuhimu wa uhuru wa uchaguzi wa wananchi kwa serikali ya kidemokrasia iliyowekwa madarakani na wananchi, mara tu baada ya kufikiwa mapinduzi nchini, alisema bila kupoteza wakati kwamba mfumo uliopasa kutawala nchini hapa ulitakiwa kuchaguliwa na wananchi ambapo pia Jamhuri ya Kiislamu iliasisiwa kwa kupigiwa kura ya asilimia 98 ya wananchi. Katika uwanja huo aliipa umuhimu mkubwa haki ya wananchi kuchagua viongozi wao ambapo hata katika mazingira magumu au hata wakati wa kujiri vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, ambapo miji mingi ya Iran ilikuwa ikishambuliwa kwa ndege za kivita za utawala wa Baathi wa Saddam, Imam Khomeini kamwe hakuruhusu wananchi kuacha kushiriki zoezi la upigaji kura.

Saddam ambaye alikuwa kibaraka wa Wamagharibi na ambaye aliishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa amri ya Wamagharibi hao

 

Isitoshe, katika kuelekea ushindi wa Mapinduzi na ukiwa umebakia muda wa mwezi mmoja tu, alikutaja kufanyika uchaguzi huru na wa haki kuwa suala muhimu ambalo lingeainisha mustakbali wa serikali ya baadaye nchini hapa. Imam alisema: “Kwanza kabisa tunatangaza vipaumbele muhimu vya baadaye vya serikali kwamba inatakiwa kufanya haraka kuandaa mazingira ya uchaguzi huru.” Baada ya hapo ikiwa imepita wiki moja tu Imam Khomeini (MA) alisema: “Moja ya majukumu muhimu ya pamoja baada ya kuanguka utawala wa Shah, ni kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru ambao hautaingiliwa na dola lolote au ushawishi wa tabaka au kundi lolote lile.” Hotuba ya tarehe 18/10/1357.

 

**********

Ndugu wasikilizaji kuandaliwa anga ya uhuru wa kisiasa kwa wanawake na kuwafanya waweze kunufaika na haki yao ya uraia wa Iran kwa ajili ya ushiriki wao katika maamuzi ya nchi yao, ni moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele na Imam Khomeini (MA) kuhusiana na suala zima la uhuru. Sambamba na kuashiria dhulma iliyokuwepo katika kipindi cha Mohammad Reza Shah, kuwahusu wanawake na pia kwa kuzingatia misingi ya dini ya Kiislamu ya kuinua nafasi ya wanawake kijamii na kisiasa, Imam (AM) alitupilia mbali madai ya baadhi ya watu kwamba utawala wa Shia ungepelekea wanawake kutengwa kisiasa na kijamii. Imam alisema: “Ushia si tu kwamba hauwatengi wanawake katika ulingo wa kijamii, bali wanawake ni wenye nafasi kubwa ya kibinaadamu katika jamii.” Hotuba ya tarehe 24/8/1357. Akijibu swali kuhusu nafasi ya wanawake katika utawala wa Kiislamu alisema: “Wanawake wana uhuru halisi wa kushiriki katika masuala mengi ya nchi, na si kama alivyotaka Shah.” Hotuba ya tarehe20/10/1357.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 16 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini. 

 

 

Tags