Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-20
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 20 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia umuhimu wa kutojihusisha kwa namna yoyote majeshi na vyombo vyote vya usalama vya nchi katika masuala ya kisiasa na uchaguzi, tukasema kuwa, Imam Khomein (MA) aliamini kwamba ni kosa kubwa kwa vyombo hivyo kujihusisha na masuala ya kisiasa nchini Iran. Katika kipindi cha leo tutazungumzia nafasi chanya ya mwanamke katika shughuli na kazi zote za ujenzi wa taifa kuanzia mwanzo wa Mapinduzi na baada yake hivyo kuweni pamoja nami hadi mwishi wa kipindi hiki.
Ndugu wasikilizaji, licha ya kwamba kuendelea kubakia maisha ya mwanadamu daima kunategemea nafasi chanya ya wanawake, sawa sawa majumbani au katika jamii, lakini katika vipindi kadhaa vya historia, jamii nyingi za wanawake, zimekuwa katika dhulma na ukandamizaji mkubwa. Aidha katika maeneo mengi ya dunia haki za wanawake zimekuwa zikipuuzwa, na zaidi ya hayo katika sekta ya haki za binaadamu, haki za wanawake na matukufu yao yamekuwa yakikiukwa waziwazi.
Hata kama katika baadhi ya jamii kumefanyika juhudi tofauti kwa ajili ya kuzingatiwa haki za wanawake, lakini matukufu yao bado yanaendelea kupuuzwa, ambapo mwanamke amekuwa akitumiwa kama chombo tu cha kufikia maslahi ya kiuchumi, kisiasa na kukidhi matamanio ya kimwili. Mbali na kufanyika juhudi kubwa za kifikra na kisiasa kwa ajili ya kufikiwa haki na kuhuishwa utukufu wa wanawake, lakini bado wanawake hawajaweza kufikia nafasi yao halisi na tukufu katika jamii. Kuharibiwa nafasi halisi ya wanawake katika jamii kumefanywa kwa kiasi kikubwa na watu wa matabaka tofauti katika nyuga tofauti za mtu binafsi na kijamii. Mbali na hayo, kufurutu ada katika kudai usawa, kuwalinganisha na kuwafananisha wanawake na wanaume, kumepelekea kupotezwa haki na sifa zao za kifizikia, kimaumbile na kimaadili katika jamii.
*********
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 20 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu uadilifu wa vyombo vya mahakama kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika anga hiyo, kubainishwa nafasi ya mwanamke kupitia maneneo ya Imam Khomeini (MA) na pia katika malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Ndugu wasikilizaji, Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofikia ushindi hapo mwaka 1979 nchini Iran, hayakupelekea kupatikana mabadiliko ya mfumo wa kisiasa tu nchini hapa, bali yalileta mabadiliko mapya katika nyuga za kifikra, kiutamaduni na kithamani katika jamii, ambapo wanawake walikuwa sehemu muhimu ya mabadiliko hayo. Katika mabadiliko hayo mapya nafasi ya kibinaadamu ya mwanamke, ilipewa uzingatiaji wa kipekee katika nyuga za kimaisha za mtu binafsi na kijamii. Aidha katika sisitizo la Mapinduzi ya Kiislamu, wanawake walipewa nafasi maalumu na ya juu, ikilinganishwa na nafasi waliyokuwanayo katika utawala uliopita wa kabla ya mfumo wa Kiislamu.
Malalamiko ya wananchi ambayo yaligeuka na kuwa mapinduzi dhidi ya mfumo uliokuwa ukitawala, hayakuhusu tu nyuga za kisiasa, bali hatua ya mfumo wa kifalme ya kukanyaga matukufu na pia kupuuza misingi ya kijamii hususan kushushwa nafasi halisi ya wanawake katika sekta tofauti, ni mambo yaliyopelekea waliowengi kutetea haki za wanawake Waislamu na waumini nchini hapa. Katika kipindi cha utawala wa Shah wa kwanza na wa pili ambao ulidumu kwa kipindi cha zaidi ya nusu karne, utawala ulikuwa ukifuata mitazamo ya Kimagharibi, ambapo wanawake walikuwa wakishawishiwa na kulazimishwa kufuata mitazamo hiyo, suala ambalo liliibua malalamiko mengi katika jamii.
**********
Katika mazingira hayo, Imam Khomeini (MA) akiwa Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu na chini ya kaulimbiu mpya, alitoa hotuba kwa jamii ya Iran kwa kuinua nafasi ya wanawake, ambapo kwa kufufua matukufu na misingi ya kidini na kitaifa vilivyokuwa vimekita mizizi ndani ya nafsi za wananchi, aliweza kuandaa mazingira ya uwepo mkubwa na athirifu wa wanawake katika nyuga tofauti za kisiasa na kijamii. Imam si tu kwamba alifanya juhudi za kurejesha haki za kimsingi, kisiasa na kijamii zilizopotea za wanawake, bali pia alifanya juhudi kubwa za kurejesha utukufu na nafasi halisi ya wanawake ambayo ilikuwa ikikandamizwa katika utawala uliopita.
Kadhalika mwasisi huyo wa Mapinduzi ya Kiislamu, sambamba na kufufua matukufu na misingi ya kidini ya mwanamke, alihuisha upya hadhi na utukufu wa wanawake kupitia nuru ya Uislamu, ili kuwawezesha kustafidi na haki zao za kisiasa na kijamii ndani ya nchi. Imam Khomeini aliamini kwamba, katika jamii iliyozungukwa na ujahili na dhulma, Uislamu uliwatukuza wanawake, mfano mzuri ukiwa ni Mtume Muhammad (saw) kuruzukiwa mtoto wa kike aliyekuwa na heri nyingi, ambaye ni Bibi Fatwimat Zahra (as). Katika hilo Imam Khomein anasema: “Bibi Fatwimat Zahra (as) alizaliwa katika kipindi na mazingira ambayo mwanamke hakuonekana kama ni mwanadamu, na uwepo wake ulihesabiwa kuwa aibu kwa watu wake wa karibu. Ni katika mazingira hayo yenye khofu kubwa, ndipo Mtume Muhammad (saw) akamuokoa mwanamke kutokana na ada chafu za kijahilia na kuonyesha utukufu mkubwa wa mwanamke katika jamii.
*******
Ndugu wasikilizaji, umuhimu wa nafasi ya mwanamke katika fikra na mtazamo wa Imam Khomein na pia katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ulikuwa mkubwa kiasi kwamba tarehe ya kuzaliwa Bibi Fatwimat Zahraa (as) ilitangazwa na mwasisi huyo wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni siku ya mwanamke nchini hapa.
Ndani ya siku hiyo wanaume na watoto huwa wanawakirimu wanawake na akina mama, ambapo nchini kote huwa kunafanywa sherehe katika kuenzi nafasi na juhudi zao. Imam Khomeini (MA) alikuwa mtu wa kwanza kubuni siku ya mwanamke nchini Iran kwa lengo la kuinua na kuonyesha nafasi halisi ya mwanamke katika jamii. Katika kuitaja siku aliyozaliwa Bibi Fatwimat Zahra (as) kuwa siku ya mwanamke Imam alisema: “Iwapo siku itatengwa kwa ajili ya kumuenzi mwanamke, basi ni siku gani nyingine itakayokuwa tukufu na yenye fahari zaidi kuliko siku aliyozaliwa Bibi Fatwimat Zahra (as)?....” Hotuba ya tarehe 15/2/1359.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 20 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.