Jun 23, 2019 18:03 UTC
  • Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-18

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 18 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia msimamo wa Imam Khomeini (MA) kuhusiana na nafasi chanya ya vyama na makundi ya kisiasa ndani ya nchi, na pia umuhimu wa serikali kuviandalia mazingira huru vyama hivyo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo, hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi.

Ndugu wasikilizaji Imam Khomeini (MA) sambamba na kukosoa mfumo wa kuiga nchi za Magharibi katika kuundwa vyama vya kisiasa nchini Iran, alitaka shughuli za vyama vya kisiasa nchini kuendeshwa kwa kuzingatia maslahi na manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla ambapo alisema: "Mataifa mengine yana vyama vya siasa lakini mfumo wa vyama hivyo ni wa aina nyingine. Si kwamba vinaweza kufanya kitendo ambacho kinaweza kuidhuru nchi yao." Hotuba ya tarehe 9/10/1358. Aliashiria pia madhara ya vyama vya siasa nchini Iran na nafasi ya vyama katika nchi za Magharibi katika kuanzisha umoja na uthabiti ndani ya nchi hizo na kadhalika harakazi zao katika kudhamini maslahi na manufaa ya kitaifa kwa kusema: "Tangu mwanzo kulipoundwa vyama nchini Iran kumekuwepo na aina fulani ya malumbano na ugomvi kati ya vyama hivyo, na hili linatokana na ukweli kwamba maajenabi walitaka kutumia tofauti na mivutano ya vyama hivyo kuibua migawanyiko na ghasia nchini. Walikuwa wakiunda vyama kama vile vya Demokrasia na Tudeh na kisha kuvifanya vigombane na kutumia umri wao wote katika ugomvi na uadui." Hotuba ya tarehe 3/10/1357.

Chaguzi nchini Iran zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia na utawala bora

 

Au katika sehemu nyingine hususan katika kufungamana vyama vya nchi zilizostawi na maslahi na manufaa ya kitaifa na kutoibua tofauti katika uwanja huo anasema: "Hamtaona hata mara moja vyama viwili nchini Marekani, kuwa kimojawapo kinafanya mambo yaliyo kinyume na maslahi ya nchi hiyo, bali baada ya uchaguzi kiongozi wa chama kilichoshindwa hutoa pongezi kwa rais aliyechaguliwa sambamba na kulinda umoja wa nchi. Lakini katika nchi yetu vyama vinashambuliana na kwenda kinyume na maslahi ya nchi yao." Hotuba ya tarehe 15/10/1359.

*******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 18 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Kadhalika Imam Khomein (MA) aliendelea kufafanua mambo mbalimbali ambapo akijibu swali la waandishi wa habari katika miaka ya mwamko wa Mapinduzi ya Kiislamu na kadhalika katika kipindi cha kuweka mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu sambamba na kusisitiza udharura wa kuwepo vyama huru vya ukosoaji katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, alitaja mipaka na misingi mikuu ya harakati za vyama vya kisiasa kuwa ni kulinda maslahi ya kitaifa. Imam Alisema: “Kila mikusanyiko na vyama vinavyoundwa na wananchi, viko huru kuendesha shughuli zao iwapo havitahatarisha maslahi ya wananchi na Uislamu umeyaainishia mipaka mambo hayo yote.” Hotuba ya tarehe 7/8/1357. Kadhalika mtukufu huyo alivitaja kuwa vyama vya kimchezo ambavyo vinajihusisha na shughuli za kudhoofisha mshikamano na umoja wa wananchi kwa kusema: “Umoja huu ulindeni kwa kuweka kando mchezo. Mrengo wa kimchezo uwekeni kando. Mwenyezi Mungu anajua mrengo huo unavyotoa pigo kwenu.” Hotuba ya tarehe 1/11/1357.

**********

Katika sehemu nyingine wakati wa kipindi cha mwamko wa Kiislamu na pia katika kipindi cha kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA) alisisitiza udharura wa kuundwa na kuendeshwa shughuli za vyama, huku akifahamu vyema kwamba katika harakati za mwamko wa Kiislamu, makundi na mirengo ya kisiasa haikuwa na nafasi athirifu.

Hadi leo ushindani wa kisiasa nchini Iran, ni kiigizo chema kwa nchi nyingi za dunia

 

Msimamo huo unaungwa mkono na historia kwa kuwa, kwa miaka yote ya harakati na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikuwa ikitawaliwa na mfumo wa kidikteta ambapo vyama na mirengo ya kisiasa nchini hapa ilisambaratishwa na kukandamizwa na serikali. Kwa mantiki hiyo ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulifikiwa chini ya harakati na anga isiyo na vyama vya kisiasa, bali chini ya kiongozi wa kiroho na idolojia ya kidini ya Imam Khomeini (MA) ambaye naye aliwategemea wananchi. Katika kubainisha nafasi chanya ya wananchi katika Mapinduzi ya Kiislamu na nafasi isiyo athirifu ya vyama na makundi ya kisiasa alisema: “….Ikiwa mtapitia mapinduzi yote, hamtopata mapinduzi yenye sifa mbili za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran: Mosi ni kwamba yamepatikana kwa kutumia wananchi bila uingiliaji wa vyama na mirengo ya kisiasa. Katika mapinduzi yote yaliyotokea duniani hakuna yanayofanana na mapinduzi ya Iran, kwa kuwa mapinduzi haya yalifuata idolojia ya Kiislamu. Na wote walikuwa wakisema: Tunataka Uislamu, kama ambavyo mikusanyiko yao yote ilikuwa ikizingatia sheria za Kiislamu. Hakukuwa na makundi yoyote yawe ya kisiasa au yasiyo ya kisiasa, yaliyokuwa na mkono katika harakati za mwamko huu, ambao ulikuwa mithili ya muujiza. Ulifanikiwa kutokana tu na kufungamana kwake na Uislamu.” Hotuba ya tarehe 27/3/1359.

*********

Katika sehemu nyingine, sambamba na kulinganisha Mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine ya dunia katika uga wa shughuli na nafasi ya vyama na makundi ya kisiasa mtukufu huyo alisema: “Hadi leo hamtapata mapinduzi kama ya Iran ambayo yalikuwa na matunda mengi makubwa na kusababisha hasara ndogo mno. Kwa kawaida mapinduzi hufikiwa kwa mamilioni ya watu kuuawa, kufungwa vyombo vyote vya habari na vyama vya kisiasa, huku watu wake wakifungwa jela. Hivyo hakuna mapinduzi kama ya Iran. Kwa kuzingatia kuwa wananchi karibu wote walikuwa Waislamu na ndio waliofanya mapinduzi hayo, milango yote ilifunguliwa kwa ajili ya kuwakaribisha watu wote.” Hotuba ya tarehe 26/8/1359. Misimamo ya Imam Khomeini kama kiongozi na mwasisi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ilipelekea baada tu ya kufikiwa ushindi wa Mapinduzi kuandikwa katiba na kufanyika kura ya maoni, kuundwa na kuanzishwa kwa uhuru kamili shughuli za vyama vya siasa nchini. Faslu ya 26 ya katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo iliungwa mkono kikamilifu na wananchi inasema: “Vyama, jumuiya, taasisi za kisiasa, asasi na jumuiya za Kiislamu au za jamii za wachache kidini zilizotambuliwa, zimewekewa sharti la kutokiuka msingi wa kujitawala, uhuru, umoja wa kitaifa, mipaka ya Kiislamu na misingi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hivyo hakuna mtu anapaswa kuzuiwa au kulazimishwa kushiriki kwenye shughuli za asasi hizo.”

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 18 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.