Alkhamisi, 04 Julai, 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Mfunguuo Pili Dhulqaada 1440 Hijria sawa na 4 Julai mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1267 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya kutegemewa, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW). Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan huko kaskazini mashariki mwa Iran kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17. Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia.
Miaka 243 iliyopita, wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini "Tangazo la Uhuru" wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia. Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa makazi ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 Miladia wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la Marekani. Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu za mashambani na viwandani.
Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Ufilipino vilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Marekani. Fernando Magellan mvumbuzi wa Kireno pamoja na wenzake ndio waliokuwa Wazungu wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika ardhi ya Ufilipino yaani mwaka 1521. Katika kipindi cha nusu karne baadaye, Uhispania ikawa imeidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mkoloni Muhispania alipora mali na utajiri wa Ufilipino kwa muda wa karne tatu.
Na katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marja taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia. Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Allama Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Hauza ya Kiislamu ya mji wa Najaf akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa na alikuwa mshairi. Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua. Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani ya "Min Wahyil Qur'an."