Jul 20, 2019 02:22 UTC
  • Jumamosi, 20 Julai, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 17 Mfunguo Pili, Dhul-Qaadah 1440 Hijria mwafaka na tarehe 20 Julai 2019.

Siku kama ya leo miaka 1261 iliyopita, Imam Mussa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa kutoka Madina na kupelekwa Iraq kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid. Imam Kadhim aliwasili Iraq tarehe 7 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 179 Hijria na kufungwa katika jela ya mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Ja'afar aliyekuwa mtawala wa Basra lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo. Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabi'i amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun. Hatimaye Imam Kadhim AS aliuawa shahidi na Sindi bin Shahik kwa amri ya Yahya bin Khalid Barmaki aambaye naye alitekeleza amri ya Haroun Rashid.  ***

Miaka 209 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18 Miladia, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi. ***

Colombia

Katika siku kama ya leo miaka 153iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati. ***

Georg Friedrich Bernhard Riemann

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita yaani tarehe 17 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1313 Hijria, Naser al-Din Shah Qajar mfalme wa wakati huo wa Iran aliuawa kwa kupigwa risasi katika Haram ya Shah Abdul-Adhim iliyoko kusini mwa Tehran. Mirza Reza Kermani ndiye aliyemuua Shah Naser al-Din. Kiongozi huyo alichukua hatamu za ufalme wa Iran akiwa na miaka 16 tu na ilikuwa ni baada ya kuaga dunia Muhammad Shah. Alishikilia wadhifa wa ufalme wa Iran kwa muda wa miaka 50. ***

Naser al-Din Shah Qajar

Miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 17 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu ambaye aliasisi Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qum. Alimu huyo alizaliwa katika mji wa Yazd katikati mwa Iran na baada ya kupata elimu ya mwanzo alielekea nchini Iraq ili kuendelea na masomo ambako alipata elimu na maarifa kutoka kwa maulamaa maarufu wa zama hizo na kufikia daraja ya juu ya ijitihad. Ayatullah Hairi Yazdi aliporejea Iran alihisi haja ya kuwepo chuo chenye nguvu cha elimu ya dini na kwa minajili hiyo mwaka 1340 Hijiria Shamsia alianzisha Hauza ya Qum ambayo ni Chuo Kikuu cha Kidini katika mji mtakatifu wa Qum. Hawza ya Qum ilipanuka kwa kasi na hivi sasa ni miongoni mwa vituo muhimu vya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu. ***

Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana  mdogo ambapo alianza kufanya utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha raidia hiyo na kufanya kazi bila ya kutumia waya. ***

Guglielmo Marconi

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita,  kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda. ***

Neil Armstrong

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo. Uturuki ilikuwa ikiwaunga mkono Waturuki huku Ugiriki nayo ikiwaunga mkono Wagiriki katika mzozo huo. Mashambulio ya kijeshi ya Uturuki kivitendo yakapelekea Cyprus kugawanyika katika sehemu mbili za wakazi Waturuki na Wagiriki na kuwa na serikali mbili. Sehemu ya kaskazini mwa Cyprus hadi leo imeendelea kuwa chini ya uvamizi na udhibiti wa Uturuki. Mazungumzo ya viongozi wa kaskazini na kusini mwa Cyprus sambamba na hatua za Umoja wa Mataifa za kutaka kupatikana serikali moja hadi leo hazijazaa matunda. ***

Cyprus

Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasishwa likisisitiza umuhimu wa kuhitimishwa vita kati ya Iran na Iraq. Azimio hilo nambari 598 lilijumuisha mada 10 na lilipasishwa kwa kauli moja na wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo linahesabiwa kuwa, moja ya mambo machache ambayo wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama walikubaliana katika historia ya miaka 40 ya Umoja wa Mataifa. Utawala wa Iraq ulitangaza kulikubali mara moja azimio hilo bila masharti yoyote.

 

Tags