Aug 14, 2019 12:41 UTC
  • Jumatano tarehe 14 Agosti mwaka 2019

Leo ni Jumatano tarehe 12 Dhulhija mwaka 1440 Hijria sawa na Agosti 14 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Agosti 2006, yalimalizika mapigano kati ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kutolewa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikubaliwa na pande hizo mbili. Mapigano hayo yaliyoanzishwa na utawala haramu wa Israel tarehe 12 Juni 2006, yalikuwa na lengo la kuidhoofisha na hata kuisambaratisha harakati ya Hizbullah. Kusimama kidete kwa wapiganaji wa Hizbullah dhidi ya majeshi ya Israel, kulimfanya Katibu Mkuu wake Sayyid Hassan Nasrullah apate uungaji mkono mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji shupavu wa Hizbullah askari wa Kizayuni ambao awali walikataa mpango wa kusitisha vita walilazimika kuukubali mpango huo na kurudi nyuma bila ya mafanikio yoyote.

Wapiganaji wa Hizbullah

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani alifariki dunia. Alimu huyo ni mjukuu wa Mirza Muhammad Hassan Ashtiyani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Tumbaku nchini Iran. Alizaliwa mjini Tehran na baada ya kukamilisha masomo ya awali alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq na kuhudhuria masomo ya maulama mashuhuri wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini na Sayyid Abul Hassan Isfahani. Ayatullah Muhammad Baqir Ashtiyani ameacha athari nyingi za vitabu zenye thamani kubwa katika nyanja mbalimbali.

yatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani

Siku kama ya leo miaka miaka 63 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti 1954, aliaga dunia malenga na mwandishi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Bertolt Brecht. Brecht alizaliwa mwaka 1898 Miladia katika jimbo la Ugsbourg nchini Ujerumani. Malenga na mwandishi huyo wa Kijerumani alihitimu elimu ya juu katika taaluma ya sayansi asilia (bayolojia, kemia na fikikia). Malenga huyo wa Kijerumani ameacha vitabu na picha ambazo nyingi zinaeleza kuhusu utawala wa Manazi na udhalimu waliokuwa wakiutenda. 

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, nchi ya Pakistan ilijitenga rasmi na India na kujitangazia uhuru wake. Dini tukufu ya Kiislamu iliingia Bara Hindi katika karne ya 8 na sehemu ya ardhi hiyo ambayo leo inajulikana kwa jina la Pakistan ilikuwa mikononi mwa Waislamu hadi wakati ilipokaliwa kwa mabavu na Waingereza mwishoni mwa karne ya 18. Chama cha Muslim League kikiongozwa na Muhammad Ali Jennah kilianzishwa mwaka 1906 kwa lengo la kuunda serikali ya Kiislamu baada ya kuanza harakati za wananchi wa India dhidi ya mkoloni Mwingereza. Chama hicho kilifanikiwa kuwashawishi Waislamu wa India na hatimaye kiliunda nchi ya Pakistan.

Tarehe 14 Agosti miaka 74 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti mwaka 1945 Japan ilisalimu amri mbele ya vikosi vya Waitifaki. Kwa utaratibu huo vita vilivyokuwa vimeanza mwaka 1939 kwa mashambulizi ya Ujerumani dhidi ya Poland vikafikia kikomo. Japan na Marekani ziliingia katika vita vikali Disemba mwaka 1941. Vita hivyo vilimalizika baada ya Marekani kushambulia miji ya Hiroshima na Nagasaki kwa mabomu ya nyuklia ambayo yaliua karibu watu laki mbili. Kusalimu amri huko kwa Japan kwa hakika kulihitimisha Vita vya Pili vya Dunia.

Japan ilisalimu amri kwa majeshi ya Waitifaki Vita vya Pili vya Dunia

 

Tags