Sep 18, 2019 11:23 UTC
  • Ruwaza Njema (19)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunayo furaha ya kukutana nanyi tena katika kipindi kingine cha Ruwaza Njema.

Leo kama kawaida tutajadili baadhi ya Riwaya zinazobainisha tabia njema ya Bwana Mtume (saw) ambapo sote tunatakiwa kuiga na kufuata mafundisho ya Riwaya hizo, kama tunavyoshauriwa kufanya na Qur'ani Tukufu. Leo tutazungumzia Hadithi ambazo zinatushauri tufuate na kuiga mfano mwema wa Mtume Mtukufu (saw) pamoja na Maimamu watoharifu (as) katika kuaga watu na pia namna ya kumkaribisha hujaji anaporejea kutoka mji mtakatifu wa Makka kutekeleza ibada muhimu ya Hija.  Tunaanza na Hadithi ambayo imenukuliwa na mtaalamu na mwanazuoni mashuhuri wa Hadithi al-Hurr al-Amili katika juzuu ya nane ya kitabu chake muhimu cha Wasail as-Shia akinukuu Hadithi ambayo imepokelewa na Ibn Absaat kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) kwamba alimuaga mtu mmoja kwa kumwambia: 'Ninaiweka roho, amana na dini yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kumwomba aifanye masurufu yako kuwa takwa yako na akupe heri kila unakoelekea. Kisha Imam (as) alitutizama na kusema: Hivi ndivyo alivyokuwa akimuaga Mtume (saw) Imam Ali (as) kila alipomtuma kwenda kufanya jambo fulani.'

*********

Na Hadithi tukufu zinasema wazi kwamba ilikuwa ni kawaida ya Mtume (saw) kuaga na kumwombea dua ya heri kwa Mwenyezi Mungu kila mtu aliyetoka kwa ajili ya kupata ridha Yake. Tunasoma katika kitabu cha Makarim al-Akhlaaq cha Allama Tabarsi riwaya kutoka kwa mpokezi anayesema: 'Mtume (saw) alitembea hatua kadhaa na Ja'ffar at-Twayyar alipomtuma Habasha na kumpa masurufu kwa maneno yafauatayo: 'Allahumma! Msahilishie utatuzi wa matatizo na magumu yote kwa sababu uwepezishaji wa matatizo ni sahali kwako, na Wewe ni muweza wa kila kitu. Ninakuomba umpe faraja na afya njema ya kudumu humu duniani na Akhera.' Na Mtume (saw) alimwaga mtu mmoja kwa kusema: 'Mwenyezi Mungu afanye masurufu yako kuwa takwa yako, akusamehe dhambi zako na heri ikupate kila sehemu uliyoko.'

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allah kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allah sana.

 

Ndugu wasikilizaji, na tunaona mfano huu bora wa kuaga watu sehemu nyingi katika sira na maisha ya Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume (saw) wakiongozwa na Bwana wao Muhammad al-Mustafa (saw). Imepokelewa katika kitabu cha Makarim al-Akhlaaq kwamba: 'Imam Ali, Amir al-Mu'mineen (as) alipokuwa akimuaga Abu Dhar (MA) kwa kutembea naye hatua kadhaa na baada ya kubaidishiwa katika eneo la ar-Rabadha kutokana na kuamrisha kwake mema na kukataza mabaya, pia aliagwa na Hassan na Hussein (as), Aqil bin Abi Talib, Abdallah bin Ja'ffar na Ammar bin Yassir (MA). Amir al-Mu'mineen Ali (as) aliwaambia: Muageni ndugu yenu kwa sababu ni lazima yule aliyelazimishwa kuondoka aondoke na muagaji arudi nyumbani. Hivyo kila mtu na aseme kile alichonacho moyoni. Hassan bin Ali (as) akasema: Mwenyezi Mungu akurehemu ewe Abu Dhar! Hakika watu hawa wamekupa mtihani mkubwa wa balaa kwa sababu tu umewanyima dini yako nao wakakunyima dunia yao. Watakuwa na haja kubwa iliyoje (kesho siku ya Kiama) nawe kutokuwa na haja hata kidogo na kile walichokunyima (dunia). Abu Dhar (MA) akasema:  Mwenyezi Mungu akurehemuni nyinyi Ahlul Beit, ambao sina kitu kingine ninachokipenda na kukihitajia duniani ila nyinyi. Hakika kila mara ninapokukumbukeni, humkumbuka babu yenu mtukufu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).

Imepokelewa pia katika kitabu hichohicho cha Makarim al-Akhlaaq Hadithi ya mpokezi inayosema: 'Mtume (saw) alipowaaga waumini alikuwa akisema: Mwenyezi Mungu ajaalie masurufu yenu kuwa takwa, akuelekezeni kwenye kila heri, akukidhieni kila haja, akulindieni dini na dunia yenu na akurudisheni kwangu mkiwa salama.'

 

Kuhusiana na ibada ya Hija, tunakunukulieni Hadithi ambayo imenukuliwa na msomi mkubwa wa Hadithi as-Sheikh al-Hurr al-Aamili katika kitabu chake cha Wasail as-Shia kutoka kwa Imam swadiq (as) ambaye amesema: 'Mtume alikuwa akimwambia mtu aliyerejea kutoka Makka: Mwenyezi Mungu atakabali Hija yako, akufungulie milango ya riziki na akusamehe dhambi zako.' Na Katika Riwaya inayofuata wasikilizaji wapenzi tunaona mfano wa kuvutia wa nasaha za Imam Ali (as) kwa Mahujaji akiwataka walinde baraka za suna za Mtume (saw) wanapokuwa wakitekeleza amali za Hija. Sheikh Swadouq ananukuu Hadithi ya 400 katika kitabu chake cha al-Khiswaal Hadithi kutoka kwa Imam Ali (as) kwamba aliwanasihi masahaba zake kwa kusema: 'Ndugu yenu wa dini anaporejea kutoka Makka, mbusuni baina ya macho yake mawili na mdomo wake ambao ulibusu Jiwe Jeusi, ambalo lilibusiwa na Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw), jicho ambalo alitazama kwalo Nyumba ya Mwenyezi Mungu (al-Kaaba), sehemu aliyosujudia na pia uso wake. Na mnapompongeza, mwambieni: Mwenyezi Mungu atakabali ibada zako, airehemu Sai' yako, abadilishe na kufidia gharama zako na asiijalie safari hii kuwa Hija yako ya mwisho.'

*******

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema kilichjokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka Tehran. Ni matumaini yetu kwamba mmeweza kunufaika na yale yote mliyoyasikia katika kipindi cha leo. Basi hadi wakati mwingine tunakuageni nyote kwa kusema; Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags