Jumanne, tarehe Mosi Oktoba, 2019
Leo ni Jumanne tarehe Pili Safar 1441 Hijria sawa na Oktoba Mosi 2019.
Tarehe Mosi Oktoba ni siku ya Wazee Duniani. Siku hii ulitengwa kwa ajili ya kuwakirimu na kuwaenzi watu wa tabaka hilo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hapa nchini Iran na kutokana na mabadiliko yaliyotokea baada ya Mapainduzi ya Kiislamu na utamaduni wa Kiislamu unaotawala hapa nchini wazee na watu wazima wanapewa nafasi ya juu ndani ya familia na jamii.

Siku kama ya leo miaka 1320 iliyopita, aliuawa shahidi Zaid bin Ali bin Hussein mwana wa Imam Sajjad (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Zaid bin Ali alisimama kupambana na dhulma za Banii Umayyah na kulinda matunda ya mapambano ya babu yake, Imam Hussein bin Ali (as). Baada ya mapambano ya kishujaa, Zaid bin Ali aliuawa shahidi katika mji wa Kufa nchini Iraq. Harakati ya mapambano ya Zaid ni miongoni mwa matunda ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria kwani baada ya mapambano ya siku ya Ashuraa kulijitokeza harakati nyingi baina ya Waislamu zilizopigana jihadi kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala dhalimu wa Banii Umayyah.

Siku kama yale leo miaka 1171 iliyopita, sawa na tarehe pili Safar mwaka 270 Hijiria, harakati ya mapambano za Wazanji ilifeli baada ya kuuawa kiongozi wa harakati hiyo Sahib al-Zanj. Ali Bin Muhammad maarufu kwa jina la Sahib al-Zanj ambaye alikuwa akijitambua kuwa mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alianzisha harakati ya mapambano mwaka 255 Hijiria akisaidiwa na wafuasi wake pamoja na watumwa weusi ambao walikuwa wakiitwa Wazanji, dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Abbas huko kusini mwa Iraq. Sahib al-Zanj aliwaahidi watumwa hao weusi kuwaachilia huru kutoka katika minyororo ya utumwa na kuwapa haki zao za kijamii kama watu wengine suala ambalo liliwafanya watu wa jamii hiyo kuvutiwa na harakati yake. Mwaka 257 Sahib al-Zanj aliudhibiti mji muhimu wa Basra, Iraq na taratibu akaanza kutwaa maeneo mengine ya karibu na mji huo. Katika kipindi hicho majeshi ya utawala wa Bani Abbasi yalifanya hujuma kadhaa dhidi ya Wazanji lakini hata hivyo hujuma hizo zilifeli kutokana na msimamo imara wa jamii ya watu hao weusi. Hata hivyo kutokana na matatizo ya ndani Wazanji walidhoofika sana na harakati yao iliyoendelea kwqa kipindi cha miaka 15 ikasambaratika baada ya kuuawa kiongozi wao Sahib al-Zanj.

Siku kama ya leo miaka 696 iliyopita, alifariki dunia nchini Misri, Abu Hayyan Gharnatwi, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 654 Hijiria huko Andalusia 'Uhispania ya leo' na baadaye alifanya safari katika miji mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Mwaka 679 Abu Hayyan Gharnatwi, alielekea nchini Misri ambako aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Akiwa nchini humo alijishughulisha na ufundisha na kuandika vitabu. Gharnatwi alikuwa mtaalamu wa elimu ya Qur'ani, Hadithi na sharia za Kiislamu, lakini alipata umashuhuri mkubwa katika utaalamu fasihi ya lugha ya Kiarabu. Abu Hayyan Gharnatwi ambaye mwishoni mwa uhai wake alikuwa kipofu, ameacha turathi nyingi kama kitabu cha 'Al-Idraaku Lilisaanil-Atraak' 'Tadhkiratun-Nuhaat' 'Tafsirul-Bahril-Muhit' na diwani ya mashairi.

Siku kama ya leo miaka 335 iliyopita alifariki dunia Pierre Corneille mwandishi na malenga wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 78. Pierre alipenda sana kujifunza uandishi wa tamthiliya na akafanikiwa kusonga mbele katika fani hiyo. Alifahamika kwa lakabu ya baba wa uandishi wa tamthiliya wa Ufaransa na mwasisi wa tamthiliya ya kiwango cha juu yaani (Classic Theatre).

Miaka 70 iliyopita Jamhuri ya Watu wa China ilitangazwa rasmi katika siku kama ya leo, na Mao Tse Tung akachaguliwa kuwa rais wa jamhuri hiyo. Nchi ya China yenye ustaarabu mkongwe ilikuwa chini ya udhibiti wa madola ya Ulaya kuanzia mwishoni mwa karne ya 16. Mara kadhaa Wachina walianzisha vita dhidi ya wakoloni hasa Waingereza ili kuikomboa nchi yao lakini hawakufanikiwa. Mwaka 1912 mapinduzi yaliyoongozwa na Sun Yat-Sen dhidi ya mfumo wa utawala wa Kifalme yalizaa matunda na kiongozi huyo akachaguliwa kuwa rais wa China.

Na siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, nchi ya Nigeria ilipata uhuru. Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 Miladia ardhi ya Nigeria iligeuzwa na kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya Uingereza, viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria. Mwaka 1914 Uingereza iliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ikajitangazia kuwa na utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ikajipatia uhuru katika siku kama ya leo.
