Jumamosi, Oktoba 12, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Tano Safar 1441 Hijria mwafaka na tarehe 12 Oktoba 2019 Miladia.
Leo tarehe 20 mwezi wa Mehr kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, inasadifiana na maadhimisho ya kumuenzi Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia mjini Shiraz moja kati ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu wa tafsiri ya Qur'ani, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'ani Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan. ***
Siku kama ya leo miaka 1138 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelekea nchini Misri akiwa kijana. Huko alijifunza elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1071 iliyopita yaani tarehe 13 Mfunguo Tano Safar mwaka 370 Hijria, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi, fiqhi na tafsiri ya Qurani Muhammad Azhari Harawi. Alizaliwa mwaka 282 Hijria katika eneo la Harat nchini Afghanistan. Harawi alitekwa nyara na Waarabu wa jangwani akiwa safarini kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya Hija na huko alijifunza lahaja asilia ya lugha ya Kiarabu ambayo aliitumia katika vitabu vyake. Mtaalamu huyo wa lugha ameandika vitabu vingi vya tafsiri na hadithi. Kitabu chake muhimu zaidi ni kile cha "Tahdhibul Lugha."
Miaka 527 iliyopita katika siku kama ya leo, mvumbuzi na baharia wa Kitaliano, Christopher Columbus alivumbua bara la America. Columbus alianza safari yake ya baharini kwa kutumia merikebu tarehe 3 Agosti mwaka 1492 kutoka kwenye bandari ya Palos nchini Uhispania akielekea kwenye Bahari ya Atlantic. Baharia huyo hakujua kwamba anaelekea bara America na kwa msingi huo tarehe 12 Oktoba 1492 na baada ya safari ya siku 70 baharini alipoona nchi kavu kwa mbali alidhani kuwa anakaribia Asia, kwa sababu alikua akiamini kwamba ardhi ina umbo la mviringo. Kwa msingi huo Christopher Columbus alivipa visiwa alivyokuwa amegundua jina la India ya Magharibi. ***
Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukua madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan. Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais. ***