Oct 14, 2019 02:38 UTC
  • Jumatatu tarehe 14 Oktoba 2019

leo ni Jumatatu tarehe 15 Safar 1441 Hijria sawa na Oktoba 14 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulifanyika kwa lengo la kujadili  “Ulaya baada ya Napoleon Bonaparte”.  Baada ya kujiuzulu na kubaidishwa Bonaparte mwezi Aprili mwaka 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulianza kufanyika katika siku kama ya leo katika mji mkuu wa Austria Vienna ili kuchukua maamuzi kuhusu ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika kipindi cha vita vya Bonaparte. Wakati wa kuendelea mkutano huo, Napoleone Bonaparte alikimbia kutoka mahala alipokuwa amebaidishiwa na mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 1815 kwa mara nyingine tena akashika hatamu za uongozi kwa muda mfupi, kipindi ambacho kiliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la “Utawala wa Siku 100”. Aliposhika tena hatamu za uongozi alijianda kuwashambulia maadui zake.

Mkutano wa kihistoria wa Vienna

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, kwa amri ya Adolf Hitler Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, nchi hiyo ilijitoa katika Jumuiya ya Kimataifa. Kuingia madarakani Adolf Hitler akiwa Kansela wa Ujerumani kulizushha wasiwasi mkubwa katika kila kona ya Ulaya kutokana na mipango yake ya kijeshi. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini mkataba wa amani wa Warsaw ambao ulidhibiti sana zana za kijeshi za Ujerumani, Hitler na viongozi wengine wa Kinazi walikasirishwa mno na hatua hiyo.

Adolf Hitler

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi huo ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan wa Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon.

Mauaji ya halaiki ya Wazayuni katika kijiji cha Qibya, Palestina

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, yaani tarehe 14 Oktoba mwaka 1964 Nikita Khrushchev, Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Umoja wa Sovieti aliuzuliwa kutoka katika wadhifa wake huo. Nikita Khrushchev alifanikiwa kuwa mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Chama cha Kikomonisti mwaka 1939 na baada ya kufariki dunia Joseph Stalin mwaka 1953, Nikita alijitokeza kuwa shakhsia aliyekuwa na nguvu katika umoja wa Sovieti na kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti na baadaye Waziri Mkuu wa shirikisho hilo.

Nikita Khrushchev

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 Ayatullah Muhammad Baqir Muhsini Malayeri, faqihi mkubwa wa Iran. Ayatullah Malayeri aliyekuwa mashuhuri katika hawza ya kielimu ya mjini Qum, Iran alizaliwa mjini Najaf, Iraq na katika familia ya kielimu, hapo mwaka 1285 Hijiria Shamsia. Akiwa kijana mdogo alielekea mjini Malayer, ambao ni makao makuu ya mkoa wa Hamadan nchini hapa akiwa pamoja na baba yake na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Mash'had kwa ajili ya kuendelea na masomo ya hawza. Wakati wa kuasisiwa hawza ya kielimu ya Qum, Ayatullah Muhammad Baqir Muhsini Malayeri naye alielekea mji huo na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Abdul-Karim Haeri Yazdi na Seyyed Hussein Borujerdi na kufikia daraja za juu za kielimu. Aidha Ayatullah Malayeri alitambuliwa kwa uchaji-Mungu mkubwa katika zama zake.

Ayatullah Muhammad Baqir Muhsini Malayeri

Na katika siku kama ya leo miaka 20 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere Alizaliwa Butiama huko Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa huku akiongoza chama cha (Tanganyika Africa Nation Union) TANU. Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 ziliungana Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Licha ya hayo, lakini Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere