Jumapili, Oktoba 13, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 14 Swafar 1441 Hijiria, sawa na tarehe 13 Oktoba mwaka 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 2558 iliyopita mji wa kihistoria wa Babel ulitekwa na Kourosh, mwasisi wa utawala wa kizazi cha Hakhamaneshi nchini Iran. Ili kuweza kuudhibiti mji huo ambao ulikuwa na ngome kubwa na imara, Kourosh aliamuru kubadilishwa mkondo wa Mto Tigris uliokuwa ukipita katikati ya mji wa Babel. Kwa utaratibu huo askari wa Kourosh walitumia njia ya zamani ya maji ya mto huo kuingia na kisha kuuteka mji wa Babel. Mji huo ulioko kusini mwa eneo la Mesopotamia katika Iraq ya sasa, ulikuwa katika kilele cha maendeleo na nguvu kubwa katika kipindi hicho.
Siku kama ya leo miaka 809 iliyopita alifariki dunia Abul-Mahaasin Bahaud-Din Ibn Yusuf, maarufu kwa jina la Ibn Shaddad, faqihi, kadhi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 539 Hijiria mjini Mosul, Iraq ambapo akiwa kijana mdogo aliweza kuhifadhi Qur'an na kisha elimu za Kiislamu kama vile hadithi, tafsiri ya Qur'an na visomo vya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu ambapo alifikia umahiri mkubwa katika uga huo. Baada ya hapo Ibn Shaddad alielekea mjini Baghdad na kuanza kufundisha katika shule ya serikali. Hata hivyo alifanya safari katika miji mbalimbali ya Kiislamu kwa ajili ya kuongeza maarifa yake, ambapo baada ya kufika kwake Sham (Syria ya leo) na kuandika kitabu kilichozungumzia masuala ya jihadi, adabu na hukumu zake, alimtunuku kitabu hicho Salah ad-Din Yusuf ibn Ayyub. Urafiki kati ya Ibn Shaddad na Salah ad-Din Yusuf ibn Ayyub uliendelea kiasi cha kumfanya kuwa mshauri na mwanahistoria wake ambapo katika safari za mtawala huyo na hata Vita vya Msalaba, walikuwa pamoja. Urafiki huo ndio ulimfanya Abul-Mahaasin Bahaud-Din Ibn Yusuf aweze kuandika matukio ya kipindi cha Vita vya Msalaba. Moja ya vitabu vyake muhimu kuhusiana na masuala ya historia ni kitabu kinachoitwa 'An-Nawaadirus-Sultwaaniyyah.' Miongoni mwa athari nyingine za Ibn Shaddad ni kitabu cha 'Dalaailul-Ahkaam' chenye juzuu nne na kitabu cha 'Al-Aswaa' ambacho kinazungumzia kisa cha maisha ya Nabii Musa (as) na mapambano yake na Firaun.
Siku kama ya leo miaka 434 iliyopita alizaliwa Ayatullah Mulla Muhsin Faiz Kashani, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu ya Irfan wa Iran. Ayatullah Kashani alizaliwa katika familia ya kielimu na ya ucha-Mungu. Akiwa na umri wa miaka miwili alifiwa na baba yake mzazi, hata hivyo kwa kutumia uelewa wake, aliweza kukwea daraja za kielimu kutoka kwa ami na mjomba wake. Muda mfupi baadaye alielekea mjini Isfahan ambapo wakati huo ulikuwa makutano ya maulama na wasomi wakubwa katika kipindi cha utawala wa Safawi. Akiwa mjini hapo Ayatullah Mulla Muhsin Faiz Kashani alisoma elimu ya fiqhi, hadithi na tafsiri ya Qur'an kwa maulama wakubwa kama vile Mohammad Taqi Majlisi na Sheikh Bahai. Aidha alisoma elimu ya falsafa, theolojia na tafsiri kwa maulama wakubwa wa elimu ya falsafa kama vile Mulla Sadra, Mir Fendereski na Mir Damad. Ayatullah Mulla Muhsin Faiz Kashani ameaandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni kitabu cha 'Tafsiri al-Swaf' 'Mafaatiihul-Sharaaii' 'Al-Waafi' 'Al-Mahajjatul-Baydhaa' na 'An-Nawaadiru.'
Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita, alifariki dunia mwandishi na mwanafalsafa wa Kifaransa, Joseph Arthur Gobineau. Gobineau alizaliwa mwaka 1816 mjini Paris na baada ya kumaliza masomo yake alijishughulisha na uandishi wa habari. Aidha Gobineau aliwahi kuwa katibu na balozi wa Ufaransa nchini Iran na kupata kujifunza lugha za Kifarsi na Kiarabu. Mwandishi huyo wa Kifaransa aliamini kuwa watu weupe hasa wale wenye asili ya Aryan ndio watu bora zaidi na kuhusiana na suala hilo akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na kutokuwepo usawa kati ya wanadamu. Nadharia ya kuwa kizazi cha Aryan ndicho kizazi bora zaidi kuliko vizazi vingine vya wanadamu ni moja ya sababu zilizompelekea Adolf Hitler kuanzisha Vita vya Pili vya Dunia na kuua kwa umati watu wasiokuwa wa asili ya Aryan.
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote. Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani walipasa kuhukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao. Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni.