Jumapili, Oktoba 20, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 21 Mfunguo Tano Swafar 1441 Hijiria, sawa na tarehe 20 Oktoba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 387 iliyopita alizaliwa Christopher Wren, msanifu majengo maarufu wa Uingereza. Wren alianza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Oxford na baadaye akaanza kufundisha chuoni hapo. Baada ya hapo Wren alijiunga na taaluma ya usanifu majengo na kufanya juhudi kubwa ambapo baadaye alifanikiwa kucjora ramani za miji ya Cambridge na Oxford. Ni baada ya hapo ndipo akapata umashuhuri mkubwa kiasi kwamba watu wengi walitumia ramani zake katika ujenzi. Moto uliouteketeza mji wa London mwaka 1666, ulimuwezesha Wren kupata umashuhuri zaidi katika fani ya usanifu majengo. Christopher Wren alifariki dunia tarehe 25 Februari 1723 Miladia akiwa na umri wa miaka 91.
Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Oktoba 1827 Miladia kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean. Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita yalishambulia meli za dola ya Othmania. Nchi hizo tatu za Ulaya zilifanikiwa kuziangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita wa utawala huo. Vita hivyo vilimalizika kwa kushindwa utawala wa Othmania sambamba na kusambaratishwa karibu askari wa majini wa utawala huo katika maji ya magharibi mwa Ugiriki.
Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na alijifunza mengi alipokuwa katika Chuo Kikuu cha Columbia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How We Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture" John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, muundo na rangi ya bendera ya Umoja wa Mataifa ilipasishwa. Baada ya kuasisiwa Umoja wa Mataifa kulizuka mjadala wa namna bendera ya umoja huo ilivyopasa kuwa. Hatimaye katika siku kama ya leo yaani Oktoba 20 mwaka 1947 uamuzi kuhusiana na jinsi muundo na rangi za bendera ya Umoja wa Mataifa zitakavyokuwa ukapasishwa.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Ja'afar Nazari Naqadi, mtaalamu wa elimu ya fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ank na usulu fiqhi. Ayatullah Naqadi alizaliwa mwaka 1303 Hijiria ambapo tangu akiwa na umri mdogo alikuwa na shauku ya kusoma elimu ya dini ya Kiislamu pamoja na fasihi. Akiwa na miaka 14 alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kuendelea na masomo yake ambapo baada ya kukamilisha masomo ya awali na ya wastani alianza kusoma elimu ya ngazi ya juu kabisa kwa maulama wakubwa kama vile, Akhund Khorasani, Mohammed Kazem Yazdi, Allamah Ahmad Kashif al-Ghitwaa na wengine wengi. Ni wakati huo huo ndipo pia alianza kujishughulisha na kazi ya ufundishaji katika maeneo ya kusini mwa Iraq. Ayatullah Ja'afar Nazari Naqadi ameacha athari mbalimbali kama vile kitabu cha 'Anwaarul-Alawiyyah wa Asraarul-Murtadhawiyyah' na 'Al-Qawaaniinul-Mantwiqiyyah.' Msomi huyo alifariki dunia mjini Najaf siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 64.
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika mpango wa kuibana harakati ya Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa kwa kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Mfalme Mohammad Idris al-Sanusi.