Jumatano tarehe 23 Oktoba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 24 Safar 1441 hijria sawa na Oktoba 23 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita, Sahib bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mtajika sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al-Muhiit" chenye juzuu saba.
Miaka 147 iliyopita, aliaga dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa. Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi na kuacha athari maarufu katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Miaka 42 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama ilizofanywa na askafi usalama wa utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, moja kati ya miji mitukufu ya Iraq. Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria shamsiya katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa ajili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27. Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.