Oct 23, 2019 23:18 UTC
  • Alkhamisi tarehe 24 Oktoba 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Safar 1441 Hijria sawa na tarehe 24 Oktoba mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita sawa na tarehe Pili mwezi Aban mwaka 1307 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti mwanafikra na mwanamapinduzi wa Iran alizaliwa huko Isfahan, moja kati ya miji ya katikati mwa Iran. Ayatullah Beheshti alilelewa katika familia ya kidini na alianza kujifunza masomo ya kidini akiwa kijana. Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Beheshti alielekea katika mji wa kidini wa Qum nchini Iran na kufunzwa na maulamaa wakubwa wa mji huo akiwemo Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Wakati huo huo, Dakta Beheshti alitumia kipawa chake kikubwa na kuamua kuendelea pia na masomo ya Chuo Kikuu na kufanikiwa kupata shahada ya uzamifu au PHD katika falsafa. Dakta Beheshti aliuawa shahidi akiwa na viongozi na shakhsiya wengine 72 wa Iran katika mkutano mwezi Tiir mwaka 1360 Hijria Shamsiya baada kundi la kigaidi la Munafiqin kuripua bomu katika mkutano huo. Dakta Behesti ameandika vitabu kadhaa kama kile cha "Mwenyezi Mungu katika Mtazamo wa Qur'ani", "Uendeshaji wa Benki na Sheria za Fedha katika Uislamu" na "Mchango wa Imani katika Maisha ya Mwanadamu."

Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti

Tarehe 24 Oktoba miaka 90 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street. Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake. Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao.

Wall Street

Tarehe 24 Oktoba miaka 74 iliyopita uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa. Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo. Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani.

Umoja wa Mataifa

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 Oktoba 1964, nchi ya Zambia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Zambia ilianza kutawaliwa na Uingereza mwaka 1888, na katika kipindi cha muongo mmoja tokea mwaka 1953 hadi 1963, Zambia ikiwa pamoja na Nyasaland na Southern Rhodesia, ziliunda Shirikisho la Afrika ya Kati. Baada ya kusambaratika shirikisho hilo, hatimaye mwaka 1964, Northen Rhodesia ilijipatia uhuru kwa jina la Zambia.

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Mirza Jawad Agha Tehrani. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 1322 Hijria katika familia ya kidini mjini Tehran na akapata elimu katika vyuo vya kidini vya Qum Iran na Najaf huko Iraq. Miongoni mwa sifa kubwa zaidi za mwanazuoni huyo ilikuwa zuhudi, ucha-Mungu na kuwapenda sana Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw). Miongoni ma vitabu vya msomi huyo ni Kanuni za Maisha na Mizanul Matalib.

Ayatullah Mirza Jawad Agha Tehrani