Jumamosi, 26, Oktoba 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Tano Safar 1441 Hijria mwafaka na tarehe 26 Oktoba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, aliaga dunia Abul-Muali Kalbasi Isfahani alimu na msomi wa elimu ya Usul. Alimu huyo aliyejulikana kwa jina la Muhammad bin Haj Muhammad Ibrahim Kalbasi alikuwa miongoni mwa wasomi na maulamaa wa Imamiya mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria. Kielimu alikuwa na daraja kubwa na ameandika vitavu pia katika nyuga mbalimbali. ***
Miaka 72 iliyopita katika siku kama hii ya leo eneo la kiistratejia la Jammu na Kashimir liliunganishwa na India baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza, na Pakistan kujitenga na India. Ilipangwa kuwa, eneo la Jammu na Kashmir lenye wakazi wengi Waislamu litajiunga na Pakistan lakini mtawala wa eneo hilo akichochewa na India na Uingereza, aliamua kuliunganisha na India na kupuuza matakwa ya wananchi. Baada ya kutangazwa habari hiyo Pakistan ililishambulia eneo hilo na kutwaa sehemu ya Jammu na Kashmir. Tangu wakati huo hadi sasa India na Pakistan zimepigana vita mara mbili juu ya umiliki wa eneo la Jammu na Kashmir na hitilafu za pande hizo mbili zingali zinaendelea. ***
Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Imam Ruhullah Khomeini baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela ya utawala wa Shah alitoa hotuba kali akishambulia vikali kitendo cha kupasishwa sheria ya Capitulation au sheria ya kuwapatia kinga ya kutofikishwa mahakamani raia wa Marekani waliofanya uhalifu nchini Iran. Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alizishambulia vikali Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Hotuba hiyo iliwaamsha wananchi na kuukasirisha utawala wa kiimla wa Shah kiasi kwamba uliamua kumuwekea vizuizi vingi kiongozi huyo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Siku chache baadaye Imam alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na baadaye Iraq. ***
Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, televisheni ya taifa ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa majaribio. Katika muongo wa 1330 Hijria Shamsia kulijadiliwa suala la kuanzishwa televisheni ya taifa ya Iran ingawa utekelezaji wa mpango huo uliakhirishwa kwa miaka mingi. Uzalishaji wa picha tena kwa masaa kadhaa tu, halikuwa jambo rahisi kwani lilihitajia fedha na uwekezaji binafsi na wa kila wiki. Ni kwa msingi huo, ndio maana Habibullah Thabit Pasal mwekezaji wa sekta binafsi akaipendekezea serikali ya wakati huo ya Iran ianzishe mnara wa televisheni, pendekezo ambalo lilikubaliwa. Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran redio na televisheni ya taifa ilibadilishwa jina na kuwa Shirika la Utangazaji la Radio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupiga hatua kubwa mno katika uwanja huo. Hii leo shirika hili lina makumi ya kanali za televisheni na radio zikiwemo zile za kitengo cha matangazo ya ng'ambo ambapo kuna makumi radio na televisheni za lugha za kigeni kama, Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, Kihispania, Kiarabu, Kihindi, Kipashto, Kiurdu, Kihausa na kadhalika. ***
Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Dakta Fat'hi Shiqaqi, akiwa huko Malta. Shiqaqi alizaliwa mwaka 1951 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza. Alihitimu masomo ya udaktari na kufanya kazi katika hospitali moja ya Baitul Muqaddas. Alianzisha harakati za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel akiwa bado kijana. Mwaka 1979 Dakta Shiqaqi alikamatwa na kusweka jela nchini Misri kwa sababu ya kuandika kitabu kuhusu harakati za Imam Ruhullah Khomeini na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Dakta Shiqaqi aliitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoainishwa na Imam Khomeini, kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu na mapambano ya jihadi dhidi ya Wazayuni huko Palestina. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, aliaga dunia Ayatullah Sayyid Abdul A'alaa Mussawi Sabzavari mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Iran. Ayatullah Sabzavari alizaliwa mwaka 1290 Hijria shamsia katika mji wa Sabzavar huko kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanazuoni huyo alianza masomo ya Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na baadaye akaendelea na masomo hayo katika mji mtakatifu wa Mash'had Iran. Alielekea katika mji wa Najaf nchini Iraq na kunufaika na elimu ya mafunzo ya Kiislamu na katika kipindi kifupi akafikia daraja ya Ijtihad. Ayatullah Sabzavari amaeandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni tafsiri ya Qur'ani yenye juzuu 30 ya Mawahibur Rahman.