Jumapili Oktoba 27
Leo ni Jumapili tarehe 28 Mfunguo Tano Safar 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 27 Oktoba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1430 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63. Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.
Siku kama ya leo miaka 1391 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo aliweza kunufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kufariki dunia Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama pamoja na ukwamishaji mambo wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah. Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufyan.
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru. Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi. Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake. Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Ayub Khan alifanya mapinduzi nchini Pakistan na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Tukio hilo lilitokea miaka 11 baada ya Pakistan kupata uhuru, ambapo Jenerali Muhammad Ayub Khan aliyekuwa mmoja wa makamanda wa jeshi alichukua hatamu za uongozi baada ya kufanya mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji damu. Kufuatia mapinduzi hayo, Iskander Mirza aliyekuwa Rais wa kwanza wa Pakistan akalazimika kuondoka madarakani. Baada ya mapinduzi hayo, Muhammad Ayub Khan ambaye alichukua nyadhifa za Urais na Waziri Mkuu alitangaza serikali ya kijeshi nchini humo. Hata kama baada ya miaka 7 Ayub Khan aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo mwaka 1965, lakini alianza kukabiliwa na mashinikizo baada ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kisiasa. Hatimaye mwaka 1969, Ayub Khan aliachia ngazi na kukabidhi uongozi wa nchi kwa Jenerali Yahya Khan aliyekuwa mkwewe.
Na siku kama ya leo miaka 46 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani, alimu mkubwa na mtaalamu wa elimu ya fiqhi. Ayatullah Zanjani alizaliwa mwaka 1308 Hijiria, huku akisomea elimu ya awali na ya juu mjini Zanjan. Baada ya hapo alielekea mjini Qum kwa ajili ya kuendelea na elimu ambapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Abdul-Karim Haeri Yazdi na Muhammad Hujjat Kuh-Kamari. Baada ya Ayatullah Muhammad Hujjat kufariki dunia, Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani alichukua wadhifa wa kuswalisha swala ya jamaa katika shule ya Fayzia. Aidha katika muongo wa 1320 Hijiria Shamsia, msomi huyo alikutana na Imam Khomeini (MA) ambapo alishirikiana naye katika vikao vingi vya kielimu. Vitabu kama vime 'Arbaiin' 'Afwaahur-Rijaal' 'Furuuqul-Ahkaam' na vitabu 20 vingine ni sehemu ya turathi za Ayatullah Sayyid Ahmad Zanjani.