Oct 31, 2019 21:41 UTC
  • Ijumaa tarehe Mosi Novemba 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na Novemba Mosi mwaka 2019.

Tarehe 3 Rabiul Awwal miaka 1000 iliyopita alifariki dunia mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul Alaa al Maarry. Alizaliwa mwaka 363 Hijria katika Syria ya sasa na baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Maarry

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, serikali ya wakati huo ya Iran ilitangaza kutofungamana na upande wowote katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Hata hivyo udhaifu wa kisiasa wa watawala wa wakati huo, matatizo ya ndani, matatizo ya kivita na kupenda kujitanua kwa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo ni mambo yaliyopelekea nchi hii kwenda kinyume na ahadi yake ya kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo. Ni kutokana na hali hiyo ndipo Iran ikajikuta katika hujuma na mashambulizi ya majeshi ya Uingereza, Urusi ya zamani na jeshi la Othmania na kuisababishia hasara kubwa.

Vita vya Kwanza vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita utawala wa kifalme nchini Uturuki ulihitimishwa rasmi na Kemal Ataturk. Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia sanjari na kudhoofika na kupoteza ushawishi wa utawala wa Othmania, Atatürk aliamua kuvunja utawala huo wa kifalme na kutwa uongozi. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Mustafa Kemal Atatürk kumaliza utawala wa kifalme wa Othmania ambao ulikuwa na misingi ya kidini. Hivyo mwanzoni alitenganisha baina ya utawala wa kisultani na cheo cha ukhalifa wa Waislamu na tarehe Mosi mwaka 1922 akavunja rasmi utawala wa kifalme huku cheo cha ukhalifa kikibakia kama cheo cha heshima tu. Suala hilo liliharakisha kuporomoka kwa utawala wa kifalme wa Othmania uliodumu kwa kipindi cha miaka 600. Baada ya kuporomoka utawala huo, uliundwa utawala wa Jamhuri na wa kisekulari hapo tarehe 29 Oktoba mwaka 1923. 

Kemal Ataturk

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, vilianza vita vya ukombozi wa Algeria baada ya kuundwa Harakati ya Ukombozi wa Algeria chini ya uongozi wa Ahmed ben Bella. Baada ya kupita miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria, hatimaye mwaka 1962 mapambano ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Algeria yalizaa matunda na nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Baada ya kutangazwa uhuru wa Algeria, Ahmed ben Bella alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Utawala wa Ahmed ben Bella ulidumu kwa miaka mitatu tu, kwani ulipofika 1965 alipinduliwa na Kanali Houari Boumediene aliyekuwa waziri wake wa ulinzi.

Ahmed ben Bella

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Aban 1359 Hijria Shamsia, alikamatwa mateka Mhandisi Muhammad Jawad Tondguyan Waziri wa Mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na maafisa kadhaa wa wizara hiyo. Operesheni hiyo ilifanywa na majeshi ya Iraq mwezi mmoja tu baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ardhi ya Iran. Mhandisi Tondguyan alikwenda kusini mwa Iran kwa shabaha ya kukagua visima na viwanda vya mafuta katika eneo hilo.

Mhandisi Muhammad Jawad Tondguyan