Jumapili, tarehe Tatu Novemba, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 5 Rabiul-Awwal 1441 Hijiria, sawa na tarehe Tatu Novemba 2019 Miladia.
Tarehe 5 Mfunguo Sita miaka 173 iliyopita kilifunguliwa chuo kikuu cha kwanza nchini Iran katika muundo na sura ya kisasa. Chuo hicho kilichojulikana kwa jina la 'Darul Funuun' kilianza kutoa mafunzo katika zama za Ufalme wa Nasiruddin Shah Qajar kwa hima ya Amir Kabiir. Lengo la kuanzishwa chuo hicho lilikuwa ni kufunza sayansi mpya na kuiwezesha Iran kupata viwanda na teknolojia ya kisasa. Miongoni mwa taaluma zilizokuwa zikitolewa katika chuo hicho ni masuala ya tiba, upasuaji, utaalamu wa madini na utengenezaji dawa. Kuanzishwa chuo hicho kulifungua ukurasa mpya katika historia ya elimu nchini Iran.
Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, nchi ya Panama ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka Colombia na siku hii huadhimishwa nchini humo kama siku ya taifa. Ardhi ya Panama iligunduliwa na kukaliwa kwa mabavu na Wahispania mnamo mwaka 1501 Miladia. Panama ilikaliwa kwa mabavu na Colombia mwaka 1821 Miladia na tangu wakati huo wananchi wa nchi hiyo walianzisha mapambano dhidi ya wavamizi wa Colombia. Mapambano hayo ya wananchi yalishadidi zaidi baada ya kuwasilishwa mpango wa mfereji wa Panama. Mwaka 1903, Panama ikafanikiwa kujitenga na Colombia na kujitawala.
Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 93 Ayatulla Mirza Hussein Husseini, maarufu kwa jina la Mirza Khalil, msomi mkubwa na mwanamapambano. Ayatulla Mirza Hussein Husseini alizaliwa yapata mwaka 1230 Hijiria katika mji wa Najaf mashariki, nchini Iraq. Msomi huyo mkuwa baada ya kuhitimu masomo ya awali na ya kati kwa baba na kaka yake, alipata pia kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Muhammad Hasan al-Najafi na Sheikh Morteza Ansari na kufikia daraja ya umarjaa wa Kishia. Hadhi ya umarjaa aliipata baada ya kufariki dunia Sayyid Mirza Bozorq Shirazi ambapo Waislamu wa Shia kutoka Iran, Iraq, Lebanon, India na maeneo mengine ya Waislamu walikuwa wakirejea kwake kiasi cha kufikia kumpa jina la Mkuu wa Hauza ya Kielimu ya Najaf. Kwa muda wote Ayatulla Mirza Hussein Husseini Khalil alijishughulisha na kazi ya kufundisha elimu ya fiqhi ambapo aliweza kulea makumi ya wanafunzi katika uwanja huo. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na 'Kitabun- fil Ijaazah' 'Kitabun fil-Ghasbi' na 'Sharhu Najaatul-Ibaad.'
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita yaani tarehe 3 Novemba 1956, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika fremu ya mashambulizi yao dhidi ya Misri, waliwaua kwa umati raia wasio na hatia katika mji wa Khan Yunis ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu. Baada ya Wazayuni kufanya mauaji hayo na kuukalia kwa mabavu mji huo, waliwaua kinyama wanajeshi 25 wa Misri na kisha kuvamia hospitali moja mjini hapo na kuwaua wagonjwa, madaktari na wauguzi wote waliokuweko hospitalini humo. Kwa ujumla wanajeshi wa utawala huo bandia waliwaua watu 275 wengi wao wakiwa akina mama wajawazito na watoto wadogo kwenye hujuma hiyo dhidi ya mji wa Khan Yunis.
Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita inayosadifiana na Novemba 3 mwaka 1996, dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jenerali Jean-Bedel Bokassa alifariki dunia. Jenerali Bokasa alizaliwa tarehe 22 Januari, 1921. Aliingia madarakani mwaka 1966 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais wa wakati huo, David Dacko. Bokasa aliitawala Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mkono wa chuma na kutenda jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kuwaua wakosoaji na wapinzani wake. Mwaka 1976 alijitangaza kuwa mfalme, cheo alichokishikilia hadi mwaka 1979 ambapo alilazimika kung'atuka madarakani baada ya mashinikizo makali kutoka kwa wananchi waliompinga na kuanzisha uasi dhidi yake. Ufaransa iliingilia kati na kumuuzulu dikteta huyo na kisha kumrudisha madarakani David Dacko