Jumatano tarehe 6 Novemba mwaka 2019
Leo ni Jumatano tarehe 8 Munguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na Novemba 6 mwaka 2019.
Miaka 1181 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Rabiul Awwal 260 Hijria, aliuawa shahidi Imam Hassan al Askari (AS) mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu SAW katika mji wa Samarra nchini Iraq. Imam Askari AS alizaliwa mwaka 232 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hadi (AS). Kipindi cha Uimamu wake kilikuwa kigumu na nyeti sana kutokana na kuzaliwa Imam wa Zama Mahdi (AS) wakati huo. Alichukua hatua kubwa za kuhuisha Uislamu na kueneza maarifa sahihi na asili ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu. Imam Hassan al Askari aliuawa shahidi kwa kupewa sumu na utawala wa Bani Abbas.

Miaka 387 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden. Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17. Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648.
Siku kama ya leo miaka 206 vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi. Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru ya nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika.
Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alichukua madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini humo na kupelekea waliokuwa wakiunga mkono utumwa kushindwa. Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita wafanyakazi wa redio na televisheni ya Iran walianza mgomo wakipinga utawala wa Shah. Mgomo huo ulifanyika kwa shabaha ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya utawala wa Shah na kuharakisha mwenendo wa kuipindua serikali yake. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la Shah walishambulia taasisi za magazeti na vyombo vya habari na kuwatia nguvuni waandishi kadhaa. Hatua hiyo ilipelekea kusitishwa uchapishaji wa magazeti yaliyokuwa yakichapishwa kwa wingi nchini.