Jumanne tarehe 12 Novemba 2019
Leo ni Juamanne tarehe 14 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na Novemba 12 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita Yazid bin Muawiya aliangamia. Yazid alikuwa mtawala dhalimu na fasiki na alitawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa. Katika kipindi cha utawala wake Yazid mwana wa Muawiya alifanya jinai kubwa na za kutisha. Miongoni mwa jinai hizo ni kumuua shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW yaani Imam Hussein bin Ali AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria, kushambulia kinyama miji mitakatifu ya Makka na Madina, kubomoa nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani Al-Kaaba na kuhalalisha mji wa Madina siku tatu ambapo askari wake waliwabaka na kuwanajisi wake na mabinti wa maswahaba wa Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita alizaliwa Ali Esfandiari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Esfandiari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Miaka 101 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulikomeshwa nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili. Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina mjini Rafah huko katika Ukanda wa Gaza. Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine 1,000.
Na katika siku kama ya leo miaka 2 iliyopita ulitokea mtetemeko wa ardhi uliokua na ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta katika mkoa wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran na maeneo ya kandokando yake huko mashariki mwa Iraq. Kituo kikuu cha mtetemeko huo wa ardhi kilikuwa umbali wa kilomita 5 kutoka mji wa Ezgeleh na kilomita 11 chini ya ardhi. Mtetemeko huo ulihisika pia katika nchi za Uturuki, Kuwait na Saudi Arabia. Karibu watu 574 waliaga dunia kutokana na mtetemeko huo wa ardhi na wengine elfu 9,388 walijeruhiwa. Watu wengine elfu sabini walipoteza makazi yao. Idadi kubwa zaidi ya watu walipoteza maisha katika miji ya Qasr-e Shirin, Sarpol-e Zahab na Salas-e Babajani.