Nov 15, 2019 23:12 UTC
  • Jumamosi, Novemba 16, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 18 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na tarehe 16 Novemba 2019 Miiladia.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, ilianza kazi ya ujenzi wa Msikiti wa Mtume mjini Madina ambao ni msikiti wa pili kwa utukufu duniani baada ya Masjidul Haram. Mtume (SAW) alitoa amri ya kujengwa Msikiti wa Madina baada tu ya kuhamia mjini humo na yeye mwenyewe alishiriki katika ujenzi wake. Kando kando ya msikiti huo kulijengwa vyumba vya Mtume na baadhi ya maswahaba zake. Mtume hakuutumia msikiti kwa ajili ya ibada tu, bali alitumia pia sehemu hiyo kwa ajili ya masuala kama kutoa hukumu baina ya watu, vikao vya mashauriano, mafunzo ya kivita na utatuzi wa masuala mbalimbali ya Waislamu. ***

Msikiti wa Madina

 

Katika siku kama ya leo miaka 432 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Sayyid Muhammad Tabatabai Amili mashuhuri kwa lakabu ya Shamsuddin, fakihi, mpokezi wa hadithi na mhakiki mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 946 Hijria katika familia yenye hadhi na iliyokuwa imeshikamana na elimu huko Jabal Amil nchini Lebanon. Alisoma masomo mengi ya awali kwa baba yake na kisha akaelekea Najaf Iraq na kufanikiwa kufikia daraja ya Ij'tihad. Sayyid Muhammad Tabatabai Amili ameandika vitabu vingi pia katika nyanja mbalimbali ambapo kitabu cha Madarik al-Ahkam Fi Sherh Sharai'i al-Islam kinatajwa kuwa moja ya vitabu vyake muhimu. ***

 

Miaka 39 iliyopita, mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq. Operesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, mabasiji na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam. Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd. ***

Ramani ikionyesha ulipo mji wa Susangerd

 

Siku kama yya leo miaka 21 iliyopita, Allama Muhammad Taqi Jaafari, mwanafalsafa na mwanafikra mkubwa wa Kiirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Kipaji chake kilidhihiri na kuchomoza tangu akiwa katika kipindi cha kuinukia kwake ambapo kabla ya kuanza shule ya msingi tayari alikuwa amejifunza Qur'ani. Akiwa shule alionekkana mwenye kipaji mno. Hata hivyo umasikini ulimfanya aache shule na kuanza kufanya kazi. Pamoja na kufanya kazi aliutumia muda wake wa ziada kusoma masomo ya dini. Allama Muhammad Taqi Jaafari ameandika vitabu vingi ambapo Tarjuma na Tafsiri ya Nahaj al-Balagha ndio kitabu muhimu zaidi cha mwanazuoni huyo. ***

Allama Muhammad Taqi Jaafari,

 

Na miaka 19 iliyopita sawa na tarehe 25 Aban 1379 Hijria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam, Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi, mmoja wa maulama na waandishi mahiri wa Kiirani. Alizaliwa huko Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na katika kiipindi cha ujana wake alielekea huko Najaf Iraq akiwa pamoja na baba yake ambaye ni Allama Amini, mwandishi wa kitabu chenye thamani kubwa cha al-Ghadir. Msomi huyo alifanikiwa pia kupata shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar cha nchini Misri. Mwaka 1350 Hijria Shamsia Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi alirejea nchini Iran na kuanza kufanya kazi ya uandishi, kufundisha na kufanya uhakiki.***