Nov 22, 2019 03:15 UTC
  • Ijumaa tarehe 22 Novemba 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 24 Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na 22 Novemba mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika taaluma ya uandishi. Katika cha ujana wake, Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo. Hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye. Aliandika kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa(as) akiwa na umri wa miaka 30. Baadaye aliandika vitabu mbalimbali vya riwaya simulizi na kupata umaarufu mkubwa katika karne ya 19.

Bi. Mary Ann Evans

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru wake. Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Tangu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943.

Bendera ya Lebanon

Katika siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas. Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo. Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.

John F. Kennedy

Na siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina. Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu. Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.

 

Tags