Nov 23, 2019 02:37 UTC
  • Jumamosi, Novemba 23, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1441 Hijria mwafaka na tarehe 23 Novemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1005 iliyopia sawa na tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijiria alifariki dunia Ali Bin Hussein Baghdadi maarufu kama Sayyid Murtadha fakihi na alimu mkubwa wa Kiislamu. Sayyid Murtadha alijulikana pia kwa lakabu ya A'lamul Huda. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za fasihi ya Kiarabu, mantiki na mashairi na kwa miaka 30 alihukumu mjini Baghdad. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20. ***

Sayyid Murtadha

 

Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, Kamati ya Kujihami Kitaifa nchini Iran iliundwa katika mji wa Qum wakati wa kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Baada ya jeshi la Russia kuvamia Iran na kusonga mbele hadi katika viunga vya mji wa Tehran na wakati huo huo kuvunjwa Bunge la Taifa, baadhi wa Wabunge, viongozi wa kidini wa ngazi za juu na wenye tajiriba, waliondoka mjini Tehran na kuelekea katika mji wa Qum na wakiwa mjini humo wakaasisi Kamati ya Kujihami ya Kitaifa. Ni wakati huo ambapo pia kulitolewa fatuwa ya jihadi dhidi ya Urusi. ***

Kuundwa Kamati ya Kujihami Kitaifa katika mji wa Qum

 

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, Jagadish Chandra Bose, msomi mtajika wa Bangladesh alifariki dunia. Jagadish alizaliwa Novemba 30 mwaka 1858 katika moja ya maeneo ambayo ni viungwa vya mji mkuu Dhaka. Miongoni mwa elimu alizokuwa amebobea Jagadish nii fizikia, sayansi ya mimea na akiolojia. Hata hivyo umashuhuri wa Jagadish Chandra Bose unatokana na kuvumbua kwake Radio na tanuri ya miale (Microwave). ***

 

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina. ***

 

Na katikak siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatima ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa. ***

André Malraux