Alkhamisi tarehe 28 Novemba 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Rabiuthani 1441 Hijria sawa na Novemba 28 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 262 iliyopita, alizaliwa William Blake mshairi na mchoraji wa Kiingereza. Blake alikuwa na mapenzi na sanaa tangu akiwa mdogo na alipofikisha rika la ubarobaro alijihusisha na kusoma vitabu vya falsafa na mashairi. Athari za mshairi huyo zilikuwa zikipingana wazi na kanisa, hali ambayo iliwakasirisha mno viongozi wa dini ya Kikristo na watawala wa Uingereza. Hadi anaaga dunia mwaka 1827, msomi huyo wa Uingereza alikuwa ameandika vitabu 13. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Marriage of Heaven and Hell, The Tiger, The Chimney Sweeper na The Lamb.
Tarehe 28 Novemba mwaka 1820 alizaliwa mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani Friedrich Engels. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani kwa jina la Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomunisti iliyotangazwa na vyama vya kikomunisti katika mkutano wao wa kwanza hapo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kubuni nadharia za kikomunisti ambazo ziliugawa ulimwengu katika kambi mbili za kisoshalisti na kibepari.
Katika siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, nchi ya Albania ilipata uhuru. Nchi hiyo ilikuwa huru miaka mingi kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, lakini baada ya kuasisiwa ufalme wa Roma ilikaliwa kwa mabavu na utawala huo. Mwaka 1501 Albania ilidhibitiwa na utawala wa Othmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 19 utawala huo ulidhoofika na kupoteza nchi za Balkan ilizokuwa ikizitawala na kwa juhudi za wapigania uhuru, hatimaye mwaka 1912 Albania ikajipatia uhuru.
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita Mauritania ilitangaza rasmi uhuru wa nchi hiyo. Mauritania ilikuwa ikikoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 Miladia. Baadaye Uholanzi na Uingereza ziliivamia nchi hiyo na mwaka 1903 Mauritania ikawa koloni la Ufaransa. Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini wananchi wa Mauritania walipiga kura ya maoni wakitaka kuasisiwa utawala wa jamhuri ya mamlaka ya ndani. Na hatimaye mwaka 1960 Mauritania ilipata uhuru kamili baada ya kusainiwa makubaliano kati yake na serikali ya Ufaransa.
Miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo Iran ilidhibiti visiwa vitatu vya Tombu Kubwa, Tombu Ndogo na Bu Musa baada ya kuondoka vikosi vamizi vya Uingereza katika maeneo hayo. Uingereza iliondoka katika visiwa hivyo vitatu vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi katika fremu ya mpango wa nchi hiyo wa kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Bahari ya Mediterranean na Ghuba ya Uajemi kutokana na matatizo ya kisiasa na kiuchumi yaliyokuwa yakiisumbua nchi hiyo.