Nov 30, 2019 01:02 UTC
  • Jumamosi, 30 Novemba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 3 Mfunguo Saba, Rabiu Thani 1441 Hijria sawa na tarehe 30 Novemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 352 iliyopita, Jonathan Swift mwandishi mashuhuri wa Ireland alizaliwa huko Dublin mji mkuu wa nchi hiyo. Swift alishiriki pakubwa katika harakati za ukombozi wa Ireland. Baadaye, Jonathan Swift alianza kujishughulisha na kazi ya uandishi. Swift alifariki dunia akiwa na miaka 78. ***

Jonathan Swift

 

Katika siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, alizaliwa Theodor Mommsen mwanahistoria na mtafiti wa Ujerumani. Baada ya kumaliza masomo, Mommsen alijishughulisha na utafiti kuhusiana na vitabu tofauti na athari zilizobakia za tamaduni za zamani. Miongoni mwa vitabu vyake maarufu zaidi ni kitabu kinachoitwa 'Historia ya Roma ya Kale' ambacho ni kitabu kamili cha historia kuhusiana na mji wa Roma. Mwanahistoria huyo wa Ujerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi hapo mwaka 1902 Miladia na kufariki dunia mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 86. ***

Theodor Mommsen

 

Miaka 184 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Mark Twain mwandishi mashuhuri wa Kimarekani. Twain alikipitisha kipindi cha utoto na ubarobaro wake na matukio yasiyo ya kawaida ambayo baadaye yalikuja kuwa maudhui kuu ya vitabu vyake. Mark Twain alikuwa mwandishi mwenye utani na mzaha. Aliandika visa na simulizi nyingi kwa ajili ya watoto na vijana wadogo ambapo tunaweza kuashiria hapa vitabu vyake viwili vya The Andventures of Tom Sawyer na (Matukio Yasiyo ya Kawaida ya Tom Sawyer) The Prince and The Pauper (Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Ombaomba). Mwishoni mwa umri wake Mark Twain alikumbwa na ukata na umasikini mkubwa na hatimaye akaaga dunia mwaka 1910 baada ya kuugua.  ***

Mark Twain

 


Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, alifariki dunia jijini Tehran Ayatullah Mirza Abul-Qassim. Kalantar Tehrani. Alikuwa alimu, msomi na fakihi mahiri wa elimu za nakili na akili. Kalantar alipoanza masomo yake kwa muda fulani alisoma kwa walimu mahiri wa Hawza ya Najaf (Chuo Kikuu cha Kidini). Baadaye alisoma kwa maulamaa wakubwa kama Sheikh Murtadha Ansari na kupata daraja ya Ijtihad. Kalantar Tehrani alikuwa mwanazuoni mashuhuri mjini Tehran na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alikuwa na nafasi maalumu baina ya watu. ***

Ayatullah Mirza Abul-Qassim.

 

Miaka 119 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Oscar Wilde, mwandishi na malenga mahiri wa Ireland. Wilde alizaliwa mwaka 1854 katika familia iliyokuwa na mapenzi maalumu na masuala ya kiutamaduni na Sanaa. Baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu. Oscar Wilde alianza kujihusisha na taaluma ya uandishi akiwa katika rika la ujana na katika kipindi kifupi cha umri wake alifanikiwa kuandika vitabu mbalimbali vilivyokuwa na madhumuni ya riwaya, mashairi na maigizo. Baadhi ya vitabu vya Oscar Wilde ni The Model Millionaire, The Soul of Man Under Socialism na The Canterville Ghost. ***

Oscar Wilde

 

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, nchi ya Barbados ambayo kijiografi ipo Amerika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru. Siku ya leo ya Novemba 30 inajulikana nchini humo kama siku ya taifa. Barbados ambayo ni nchi ndogo ya Amerika ya Kati ilivumbuliwa na Uhispania katika karne ya 15 na kukaliwa kwa mabavu na nchi hiyo ya Ulaya. Karne moja baadaye Ureno ikadai mamlaka huko Barbados. Hadi kufikia karne ya 17 nchi mbili hizo za kikoloni yaani Ureno na Uhispania ziliwatimua nchini humo wakazi wa asili wa ardhi hiyo. Barbados ina ukubwa wa kilomita mraba 431 na ipo baina ya Bahari ya Caribbean na kaskazini mwa Amerika ya Kusini na mji mkuu wake ni Bridgetown. ***

Bendera ya Barbados

 

Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, aliaga dunia katika mji wa Cairo Misri, Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad, mmoja wa waalimu na maqarii wakubwa wa Qur'ani Tukufu. Abdul-Basit alianza kujifunza Qurani Tukufu tangu akiwa mdogo na alipofikia umri wa miaka 12 akafanikiwa kupata tunzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani. Ustadh Abdul-Basit katika maisha yake alijishughulisha na usomaji wa Qurani Tukufu na kutunukiwa zawadi na tunzo muhimu katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu kwenye nchi mbalimbali za Kiislamu, sambamba na kuwavutia Waislamu wengi kwenye kusoma maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Abdul Basit ameacha kanda nyingi za sauti yake nzuri ya Qur'ani Tukufu. ***

Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad

 

Na siku ya leo inayosadifiana na tarehe 9 Azar kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsiya huadhimiwa hapa nchini Iran kama siku ya kumbukumbu ya Sheikh Mufid, alimu, msomi na mwanafikra mkubwa wa Kishia. Alimu huyu ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Mufid, jina lake kamili ni Muhammad bin Nu'man na alizaliwa huko Baghdad mwaka 336 Hijria. Alionyesha kipaji kikubwa cha masomo na ufahamu tangu akiwa katika rika la utoto na ni katika kipindi hicho pia alipoanza kusoma masomo ya Kiislamu. Sheikh Mufid ameandika vitabu vingi ambavyo vinakadiriwa kufikia 200. Al'Alam, Amali na Irshad ni baadhi ya vitabu mashuhuri kwa Sheikh Mufid. Alimu huyu amezikwa huko Kadhmein Iraq. ***

Sheikh Mufid