Jumatano tarehe 5 Februari 2020
Leo ni Jumatano tarehe 10 Jamadithani 1441 Hijria sawa na Februari 5 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Imamu Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi ya Kiislamu; hatua ambayo ilichukuliwa muda mfupi kabla ya ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika amri yake hiyo, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza malengo na mipango ya Mapinduzi ya Kiislamu na akaitaka serikali ya muda ifanye hima kwa ajili ya kufikiwa malengo hayo. Aidha katika amri hiyo, aliainisha jukumu kuu la serikali ya muda ambalo lilikuwa kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mfumo wa kisiasa utakaotawala hapa nchini, kuandaa uchaguzi na kuunda Baraza la Waasisi kwa ajili ya kutunga Katiba na kufanyika uchaguzi wa kwanza wa Bunge.
Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo shirika la ujasusi la Marekani CIA lilikiri kwamba, limefeli katika kutazamia masuala na mkondo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Maafisa wa CIA walikiri kwamba, shirika hilo la ujasusi la Marekani limeshindwa na kufeli katika kutoa utabiri kuhusu masuala ya Iran. CIA ilisema: Kitu ambacho hatukutazamia ni kuona mzee mwenye umri wa miaka 78 akiwaunganisha pamoja watu wa Iran baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 14.
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle. Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo. Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo." Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza."
Miaka 814 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia arifu na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Fariduddin Attar Naishaburi. Attar Naishaburi alizaliwa karibu mwaka 513 Hijria Qamaria katika eneo la Naishabur na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafsi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu ya kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo.
Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantiqut Twair."