Ijumaa tarehe 7 Februari 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 12 Jamadithani 1441 Hijria sawa na Februari 7 mwaka 2020.
Miaka 798 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abul Hassan Ali bin Abdu Samad Hamdani, mtambuzi wa lugha, fakihi na mfasiri wa Qur'ani katika karne ya 7 Hijria. Alizaliwa huko Sakha katika viunga vya Misri na akaondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Sakhawi. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, Abul Hassan Ali bin Abdu Samad alielekea Sham na kuishi Damascus katika Syria ya leo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali katika elimu za Tajweed, teolojia na hadithi. Baadhi tu ya vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na al Jawahir na Sifrus Sa'ada.

Siku kama ya leo miaka 542 iliyopita, alizaliwa Thomas More, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Uingereza. Mwanzoni More alisomea sheria na baada ya kujiunga na Bunge alipewa mazingatio na malkia wa wakati huo na kutunukiwa hadhi ya Ulodi. Hata hivyo Thomas More alitofautiana kinadharia na mfalme wa wakati huo wa Uingereza na hivyo akatiwa jela na kuhukumiwa kifo. Hatimaye More alinyongwa mnamo tarehe sita Julai mwaka 1535 akiwa na umri wa miaka 57.
Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, alizaliwa mjini Newcastle, Edward Granville Browne, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, mtafiti na mwanafasihi wa Uingereza. Awali Browne alihitimu taaluma ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Hata hivyo kutokana na kupendelea kwake tamaduni za mashariki mwa dunia alifanya safiri nchini Iran akiwa na umri wa miaka 25. Mtafiti huyo aliitaja lugha ya Kifarsi kuwa chombo bora ya kunakili fikra na tamaduni za Wairan kuelekea maeneo mengine ya dunia. Ni kwa msingi huo ndio maana akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na historia na utamaduni wa Wairani. Mwishoni Edward Granville Browne alijikita katika kufundisha lugha ya Kifarsi na Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cambridge na alifariki dunia mwaka 1926 akiwa na umri wa miaka 54.
Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi dogo ya Grenada iliyoko katika Amerika ya Kaskazini ilijipatia uhuru. Kisiwa hicho kiligunduliwa mwaka 1498 na Christopher Columbus mvumbuzi wa Kihispania na ikaunganishwa na nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1674 Ufaransa ikaidhibiti Grenada. Baada ya takribani karne moja yaani mwaka 1783, Waingereza waliifanya Grenada kuwa koloni lao na hali hiyo ikadumu kwa takribani karne mbili. Hatimaye mwaka 1974 na katika siku kama ya leo, Grenada ikajikomboa na kujipatia uhuru.
Tarehe 18 Bahman miaka 36 iliyopita aliuawa Jenerali Gholam-Ali Oveissi aliyehusika na mauaji ya wananchi wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Jenerali Oveissi ambaye alikuwa Kamanda Mkuu wa jeshi la utawala wa kifalme wa Shah alihusishwa na mauaji ya wananchi wa Iran mwaka 1962 na 1978 katika vuguvugu la wananchi wa Iran la kutaka kuanzishwa Jamhuri ya Kiislamu na kuuondoa madarakani utawala wa dhalimu wa kifalme. Oveissi alikimbia nchi mwezi mmoja kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hata kabla ya Shah Pahlavi kutoroka nchi. Mwezi mmoja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jenerali Oveissi alifanya jitihada za kuwakusanya tena waungaji mkono wa utawala wa kifalme nchini Iran na kutoa dharba kwa Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo njama hizo zilishindwa na hatimaye kibaraka huyo wa Shah aliuawa katika siku kama hii leo akiwa Paris nchini Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita aliaga dunia Hussein bin Talal mfalme wa zamani wa Jordan kwa ugonjwa wa saratani. Alizaliwa mwaka 1935 huko Amman mji mkuu wa Jordan na kuhitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Uingereza. Mfalme Hussein alikalia kiti cha usultani huko Jordan mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 19 baada ya kuuawa babu yake, Mfalme Abdallah na baada ya baba yake Amir Talal kukalia kiti cha uongozi kwa miezi kadhaa tu. Mapinduzi na mauaji mengi yalitokea wakati wa usultani wa mfalme Hussein bin Talal huko Jordan.