Feb 09, 2020 02:41 UTC
  • Jumapili, tarehe 9 Februari, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 14 Mfunguo Tisa Jamadu th-Thani 1441 Hijria, sawa na tarehe 9 Februari 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 936 aliyopita, alifariki dunia msomi na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiiran Abu Hamid Muhammad Ghazali Tusi, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Baada ya kuaga dunia baba yake, yeye na kaka yake, Ahmad walilelewa na Ahmad bin Radkani. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama "Ihyau Ulumud Din," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme."

Abu Hamid Muhammad Ghazali Tusi

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Habibullah Rashti, mmoja wa maulama na maraajii wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Katika kujiendeleza kielimu, alifunga safari kuelekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama zake kama vile Sheikh Morteza Ansari ambapo taratibu alikwea marhala za kielimu na hata kufikia umarjaa wa kidini. Kitabu cha 'Badaaiul-Afkaar' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo.

Ayatullah Mirza Habibullah Rashti

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, yaani sawa na tarehe 20 Bahman 1357 Hijiria Shamsia, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini. Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah. Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la vibaraka hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangushwa utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza.

Shambulizi la vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran dhidi ya moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita sawa na tarehe 9 Februari 1984, alifariki dunia Yuri Andropov, mmoja wa viongozi wa Urusi ya zamani. Andropov ambaye alikuwa mwanasiasa mkubwa wa Urusi ya Zamani alizaliwa tarehe 15 Juni 1914 Miladia ambapo akiwa kijana alijiunga na harakati za kisiasa sambamba na kujiunga na chama cha Kikomonisti. Mwaka 1953 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa balozi wa Urusi ya zamani nchini Hungary ambapo wakati nchi yake ilipoivamia Hungary mwaka 1956, alitwaa uongozi wa operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na kutekeleza ukandamizaji na umwagaji damu dhidi ya wapigania uhuru wa Hungary. Mwaka 1967 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Urusi ya zamani KGB ambapo aliendelea kuliongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka 15 yaani hadi alipofariki dunia Leonid Brezhnev, Kiongozi wa wakati huo wa Urusi ya zamani hapo mwaka 1982. Miezi saba tangu kiongozi huyo afariki dunia, Andropov aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani, ambacho ni cheo cha juu kabisa nchini humo. Aidha aliendelea kusimamia uongozi wa chama hicho kwa kipindi cha miaka 15, hadi alipofariki dunia. Katika kipindi chake kuliongezeka mashindano ya uundaji wa silaha za nyuklia.

Yuri Andropov

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi. Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq. Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq.

Operesheni ya Walfajir 8

Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa nchini mhumo. Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.

Bendera ya Algeria