Feb 15, 2020 04:12 UTC
  • Jumamosi, 15 Februari, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1441 Hijria mwafaka na tarehe 15 Februari 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1449 iliyopita, alizaliwa Bibi Fatima Zahra, binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Bibi Fatima Zahra alilelewa katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora na mwongozo wa baba yake Mtume Muhammad (saw) na hivyo kuweza kufikia daraja za juu za ukamilifu. Bibi Fatima (as) alikuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili baba yake kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria, Bibi Fatima Zahra alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu katika sherehe ndogo iliyosimamiwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Vilevile Bibi Fatima akiwa na Imam Ali alifanikiwa kulea shakhsia adhimu kama Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as). Mbali na majukumu ya kulea familia, Bibi Fatima Zahra, alijishughulisha pia na malezi ya jamii. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 456 iliyopita, alizaliwa msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia, Galileo Galilei katika mji wa Pisa. Alisoma fasihi hadi alipokuwa na umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu, Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba, sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Muislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba, ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa kafiri na akahukumiwa kifungo cha maisha cha nyumbani. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake. ***

Galileo Galilei

 

Miaka 238 iliyopita katika siku kama ya leo, vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi saba, vilikuwa mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. Ijapokuwa Ufaransa ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na kuikoloni nchi hiyo na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa mkoloni mkuu huko Bara Hindi. ***

Vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India

 

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alizaliwa Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979. ***

Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al-Musawi Khomeini,

 

Na miaka 31 iliyopita, Jeshi Jekundu la Shirikisho la Urusi ya zamani lililazimika kuondoka nchini Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya mujahidina wa Kiislamu. Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa kuizatiti na kuipa nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. Hatua hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House) ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko Afghanistan. Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na kuyafukuza majeshi ya Urusi katika ardhi yao. ***

Afghanistan