Feb 15, 2020 08:35 UTC

Assalaamu Alaykum Wapenzi Wasikilizaji wa Radio Tehran, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale mlipo hususan huko nyumbani Afrika Mashariki.

 

Karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki kipya chenye anuani isemayo: Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katikka Uislamu. Katika kipindi cha historia ya miaka 1200 ya Uislamu baada ya kuondokewa na Maimamu watoharifu 11 ambapo wa kumi na mbili yupo ghaiba, walijitokeza maelfu ya wanazuoni, mafakihi na wasomi wakubwa katika Ulimwengu wa Kishia, ambapo kwa nuru ya elimu yao, waliweza kuifanya njia ya uongofu wa Mwenyezi Mungu ibakie kuwa na mwanga na nuru.

Katika mfululizo wa kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa kishia Katika Uislamu tunalenga kubainisha, historia ya wanazuoni na maulamaa hawa iliyojaa harakati, athari na mchango wao ambao umeweza kusukuma mbele gurudumu la malengo ya Mwenyezi Mungu, maulamaa na wanazuoni ambao walitumia sehemu kubwa ya umri na maisha yao kuhudumia Uislamu. Aidha tutachambua pia sifa zao pamoja na daraja zao za Kiirfani pamoja na athari zao za kimaandiko walizoziacha ambazo zimeondokea na kuwa turathi na dafina za kielimu kwa vizazi vilivyokuja baada yao. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa sehemu hii ya kwanza ya mfululizo huu.

السلام علیک یا اهل بیت النبوه

 

Wapenzi wasikilizaji Maulama na wanazuoni wa dini wana nafasi na daraja ya juu katika utamaduni wa Kiislamu. Hata katika jamii zetu tunazoisha inafahamika wazi kwamba, mjinga na mjuuzi hawawezi kulingana. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 9 ya Surat Zumar:

Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua?

Mtume Muhammad (saw) ambaye ni mjumbe wa mwisho wa Allah kuleta risala kwa walimwengu, anawataja Maulamaa na wanazuoni kama taa ya ardhini na warithi wa Mitume. Uislamu ndio dini ya mwisho ya Mwenyezi Muungu ambapo baada ya Mtume Muhammad (saw) Mwenyezi Mungu hakumtuma na hatatuma Mtume mwingine kwani Muhammad ndiye aliyekuwa Mtume wa mwisho. Mtume wa mwisho ambaye alikuwa mja kama waja na wanadamu wengine aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake baada ya kuishi kwa miaka 63.

Hata hivyo mafundisho yake yamebakia na yatabakia kuwa hai hadi milele.  Uwepo wa Maimamu 12 Maasumu wenye nuru kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume zaidi ya karne mbili baada ya kudhihiri Uislamu, kulipelekea mche wa Uislamu uendelee kustawi na kusalimika na upepo na tufani ya matukio pamoja na mafuriko yenye uharibifu ya watu wa nifaki na wenye upotofu. Hata hivyo ulimwengu wa mwanadamu ukiwa na lengo la kuhifadhi dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu uligharamika pakubwa na kwa roho za mifano ya watu wakamilifu zaidi yaani Maimamu Maasumu (as).

 

Imam wa Kumi na Mbili yaani Muhammad Mahdi (atfs) ameghibu na haionekani katika upeo wa macho ya watu kwa amri na irada ya Mwenyezi Mungu. Sababu ya kuwa ghaiba Imam Mahdi ni katika siri za Mwenyezi Mungu ambazo zinafichuka mara atakapodhihiri.

Kuhusiana na thamani, adhama na daraja ya aalimu na nafasi yake kinatutosha Kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani ambapo wanazuoni na wenye elimu wametajwa kama mashuhuda baada ya Mwenyezi Munguu na Malaika kwamba, Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Aya ya 18 ya Suran al-Imran inasema:

Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana Mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana Mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Maasumina (as)

 

Katika Aya hii, wanazuoni ambao wamekunywa kinywaji cha Tawhidi na mioyo yao inang'ara kwa nuru ya imani wametajwa baada ya Mwenyezi Mungu na Malaika, jambo ambalo linadhihirisha daraja ya juu waliyonayo.

Imam Sajjad as anasema kuwa: Mwenyezi Mungu alimshushia Wahyi Nabi Daniel akimwambia: Mja ninayemchukia zaidi nii mjinga, ambaye anaidogosha haki ya wasomi na anayeacha kuwafuata.

Nafasi maalumu waliyopatiwa Maulamaa na Uislamu si ya hivi hivi, dini ambayo kwa mujibu wa irada ya Mwenyezi Mungu ndio ya mwisho na kamili zaidi miongoni mwa dini za mbinguni ambayo ina miongozo yote kwa ajili ya saada na ufanisi wa maisha ya mwanadamu. Dini hii ambayo huenda ikaendelea kubakia kwa mamia au maelfu yya miaka bila ya kuweko Mtume, inahitajia Maulamaa weledi na wenye utambuzi na wacha Mungu ili waweze kutoa majibu kwa wanadamu kwa mahitaji mapya ya mwanadamu huyu.

 

Mwenyezi Mungu katika Qur'ani amebainisha kanuni na misingi jumla isiyobadilika kwa ajili ya saada ya milele kwa mwanadamu, ili wanadamu kwa kutumia Wahyi na akili na kwa kuzingatia mazingira ya zama zao waweze kugundua hukumu za masuala madogo madogo lakini muhimu katika nyanja mbalimbali za maisha.

Ugunduzi huu unahitajia ubobeaji wa kila upande wa vyanzo vya dini, imani imara na nguvu ya akili, ambapo hayo hayawezekani isipokuwa kwa kuweko malezi sahihi na juhudi maradufu, mtawalia na zisizokoma.

 

Kwa hakika tawfiki hii hapati kila mtu. Kwa hakika Maulamaa wa dini ni wale watu ambao wana irada na imani thabiti na imara na hayo ni matunda ya umri na maisha yao yaliyyojaa juhudi na idili kubwa ya usiku na mchana kwa ajili ya kutoa mchango mkubwa katika Uislamu na kuifanya dini hii ibakie.

Wapenzi wasikilizaji kama tulivyotangulia kusema, katika mfululizo wa vipindi hivi, tutajaribu kubainisha historia ya wanazuoni na maulamaa hawa iliyojaa harakati, athari na mchango wao ambao umeweza kusukuma mbele gurudumu la malengo ya Mwenyezi Mungu. Aidha tutachambua pia sifa zao pamoja na daraja zao za Kiirfani kama ambavyo pia tutaangazia na kuashiria baadhi ya athari na vitabu vyao muhimu ambavyo leo ni turathi na dafina ya Waislamu.

Kwa leo nalazimika kukomea hapa nikkitaraji kwamba, mtakuwa pamoja nami juma lijalo katika safari hii ndefu ya "Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu".

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.