Jumamosi, 22 Februari, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Tisa Jamadithani 1441 Hijria mwafaka na tarehe 22 Februari 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1050 iliyopita, kwa mujibu wa riwaya mbalimbali aliaga dunia Hussein bin Ahmad Hajjaj mshairi na malenga mashuhuri wa Kishia. Hussein bin Ahmad Hajjaj aliyekuwa malenga mahiri na mwanafsihi mbobezi, aliishi zama moja na Sayyid Murtadha na Sayyid Radhi wanazuoni na wanachuoni wakubwa wa karne ya nne Hijria. Alikuwa mshairi kipenzi wa Ahlul-Baiti (as) na adui mkubwa wa maadui wa dini na ametunga beti nyingii za mashairi katika uwanja huo. Hussein bin Ahmad Hajjaj aliaga dunia katiika eneo lililopo baina ya Baghdad na Kufa na kwa mujibu wa wasia wake, Ibn Hajja alizikwa upande wa chini wa miguu Imam Mussa al-Kadhim (as) katika mji wa Kadhmein Iraq. ***
Katika siku kama ya leo miaka 349 iliyopita aliaga dunia Adam Olearius mtafiti, mwanahisabati na mtaalamu wa masuala ya Iran wa Ujerumani. Alizaliwa mwaka 1603 na baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi alianza kujishughulisha na masomo katika taaluma ya teolojia, falsafa, hisabati na fizikia katika Chuo Kikuu cha Leipzig. Adam Olearius alikusanya taarifa muhimu katika kipindi cha utawala wa Safavi nchini Iran na kuziandika katika kitabu chake kinachoelezea matukio mbalimbali katika safari zake. Alikuwa akiifahamu vizuri lugha ya Kifarsi na alikuwa na mapenzi makubwa na utamaduni na fasihi ya Kiirani. ***
Miaka 232 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Arthur Schopenhauer msomi na mwanafalsafa wa Kijerumani. Alipokuwa na umri wa miaka 17 baba yake alijiua. Arthur Schopenhauer hakuwa na uhusiano mzuri na mama yake. Jambo hilo lilimfanya awe mtu mwenye mtazamo mbaya na ajitenge na watu. Awali akiwa Chuo Kikuu alisoma taaluma ya tiba na baadaye akasoma Sayansi Asilia (Natural Science). Hata hivyo baadaye alianza kusoma falsafa na mwaka 1813 akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu (PhD). ***
Siku kama ya leo miakka 114 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar aliomba hifadhi katika ubalozi wa Russia. Kushika kasi na kupanuka wigo wa cheche za Mapinduzi ya Katiba (Constitutional Revolution) katika maeneo mbalimbali ya Iran kulipelekea kuibuka harakati ya kuikomboa Tehran ya wapigania katiba na wakafanikiwa kupata ushindi. Vikosi vya Muhammad Ali Shah Qajar vilishindwa jirani na mji wa Tehran. Hatimaye mji wa Tehran ukadhibitiwa na wapigania Katiba. Muhammad Ali Shah Qajar baada ya kuona kuwa amezidiwa nguvu na wanaharakati hao alikimbilia katika ubalozi wa Russia na kuomba hifadhi. Siku hiyo hiyo kukafanyika kikao cha dharura na Muhammad Ali Shah Qajar akauzuliwa na badala yake mwanawe Ahmad Mirza aliyekuwa na miaka 11 akatangazwa kuwa mfalme.***
Katika siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Isfand mwaka 1299 Hijria Shamsia, Uingereza ilitekeleza siasa zake za kikoloni kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran. Njama hiyo ya mapinduzi ilipangwa na maafisa wa serikali ya Uingereza waliokuwa mjini Tehran wakishirikiana na baadhi ya maafisa usalama wa mji huo. Wafanya mapinduzi waliudhibiti mji mkuu baada ya mapigano ya muda mfupi, na Ahmad Shah Qajar akalazimika kumteua Reza Khan kuwa Kamanda Mkuu wa majeshi. Miaka minne baadaye Reza Khan ambaye alikuwa akiungwa mkono na kusaidiwa sana na Waingereza kutokana na kukanamiza harakati za ukombozi za wananchi alifanywa mfalme wa Iran hadi mwaka 1320 Hijria Shamsia, ambapo aliondolewa madarakati na Waingereza wenyewe na kupelekwa uhamishoni baada ya kuegemea upande wa Ujerumani katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. ***
Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo, katika siku kama ya leo yaani tarehe 22 Februari mwaka 1958, Abul Kalam Ahmad Azad, msomi, khatibu na mwanasiasa wa India alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalam Azad alianza harakati za kisiasa akiwa na umri wa miaka 17 na harakati zake zilikuwa dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza kwa shabaha ya kuwazindua Waislamu wa India. Msomi huyo alifungwa gerezani mara kadhaa na wakoloni wa India, kutokana na hatua zake za kuchapisha na kutoa hotuba zenye kufichua ukandamizaji wa Uingereza. Baada ya India kupata huru, alichaguliwa kuwa mbunge na Waziri wa Elimu wa nchi hiyo. ***
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni ya 'Khaybar' dhidi ya majeshi ya Iraq, kwenye vita vya kulazimishwa vilivyoazishwa na utawala wa Baath wa Saddam Hussein. Katika operesheni hiyo iliyofanyika katika eneo la Hoor al Hoveyzah kusini magharibi mwa Iran, wapiganaji shupavu wa Iran walifanikiwa kuvuka maji na kukiteka kisiwa chenye utajiri mkubwa wa mafuta cha Majnoon, kilichoko karibu na mji wa Basra kusini mashariki mwa Iraq. Mbinu tata za kijeshi zilizotumika katika oparesheni hiyo ya majini na nchi kavu ya Khaibar ziliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi duniani. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Haram mbili takatifu za Maimamu al Hadi na Hassan al Askari katika mji wa Samarra nchini Iraq, ziliharibiwa vibaya kwenye mlipuko wa mabomu kadhaa. Maimamu hao ni wajukuu wa Mtume Muhammad SAW. Kitendo cha kuharibiwa sehemu kubwa ya haram hizo, kiliwakasirisha mno Waislamu hasa wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume SAW. Shambulio hilo lilifanyika kwa lengo la kuzusha vita vya ndani vya kimadhehebu kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni. Hata hivyo kuwa macho wananchi wa Iraq na viongozi wa kidini wa nchi hiyo kulisambaratisha njama hizo. ***
