Jumanne tarehe 25 Februari 2020
Leo ni Jumanne tarehe Mosi Rajab 1441 Hijria sawa na Februari 25 mwaka 2020.
Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.” Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu. Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab.

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Siku kama ya leo miaka 267 iliyopita tabibu mmoja wa Uingereza aligundua njia ya kutibu maradhi ya Ascorbate. Maradhi hayo husababishwa na upungufu wa vitamini C mwilini na kulegeza fizi za meno na hatimaye meno huanza kudondoka na kutokwa na damu nyingi wakati wa majeraha madogomadogo. Kwa kuwa zamani wafanyakazi wa vikosi vya majini na wahudumu wa meli na mabaharia ambao hawakuwa na uwezo wa kupata matunda na mboga walikuwa wakipatwa kwa wingi na maradhi hayo, ugonjwa huo ulikuja kujulikana kwa jina la ugonjwa wa mabaharia.

Katika siku kama hii ya leo miaka 36 iliyopita ndege za kivita za utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein zilishambulia miji ya Saqz, Pol-e Dokhtar na Mahabad. Utawala wa Saddam Hussein uliamua kushambulia makazi ya raia katika miji mbalimbali ya Iran sambamba na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa Kiislamu hususan katika operesheni ya jeshi la Iran iliyopewa jina la Khaibar na kipigo cha jeshi la Iraq katika visiwa vya Majnun. Makumi ya raia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.

Tarehe 25 Februari miaka 34 iliyopita dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake. Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo. Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya mwongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos alilazimika kukimbia Ufilipino.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili.Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani!