Feb 28, 2020 23:04 UTC
  • Jumamosi, Februari 29, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 5 ya mwezi Rajab 1441 Hijria sawa na tarehe 29 Februari 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1197 iliyopita kulingana na kkalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia aliyekuwa na uadui mkubwa na Ahluul-Baiti (as) kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. ***

Ibn Sikkit

 

Katika siku kama ya leo miaka 971 iliyopita, aliaga dunia Ibn Bannaa mwanazuoni na msomi wa Ulum Qur’an. Abu Ali Abdallah bin Banna alikuwa mpokezi wa hadithi na fakihi mahiri wa Kiislamu. Ibn Banna alikuwa pia mhakiki na mtafiti hodari wa taaluma za historia, akhlaq, hadithi, teolojia na lugha na ameacha athari nyingi mno katika nyanja mbalimbali. Baadhi ya wasomi wanasema kuwa, athari na idadi ya vitabu vya Ibn Banna vinafikia 150. Hata hivyo ni athari tatu tu kati ya hizo ambazo zimehifadhiwa katika maktaba kubwa ya Damascus. Mwanazuoni huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 85. ***

Abu Ali Abdallah bin Banna

 

Katika siku kama ya leo, miaka 41 iliyopita, hayati Imam Ruhullah Khomeini kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika mji wa kidini wa Qum baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Imam alipelekwa uhamishoni na utawala wa Shah hapo mwaka 1343 Hijria Shamsia baada ya matukio ya umwagaji damu ya tarehe 15 Khordad mwaka 1342. Tarehe 12 Bahman mwaka 1357 Imam alirejea nchini akitokea Ufaransa na katika siku kama ya leo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasili katika mji mtakatifu wa Qum na kuishi huko. Miezi kadhaa baadaye Imam Ruhullah Khomeini alihamia Tehran kutokana na udharura wa kuongoza Mapinduzi.***

hayati Imam Ruhullah Khomeini

 

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, Kamati ya Nia Njema ilianza kazi zake mwanzoni mwa vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kamati hiyo ilianzishwa kwa pendekezo la Mawaziri wa Jumuiya ya Kiislamu na baada ya kupasishwa na wakuu wa jumuiya hiyo ya OIC. Kamati ya Nia Njema ilikuwa na jukumu la kuhitimisha vita vya Iraq dhidi ya Iran kupitia njia ya amani. Kamati hiyo baadaye ilibadilishwa jina na kufahamika kama Kamati ya Amani. ***

Vita vya kichokozi vya Saddam Hussein dhidi ya Iran

 

Na katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, baada ya utawala wa Saddam Hussein wa Iraq kushindwa mtawalia katika medani ya vita na Iran, utawala huo wa Baath ulishambulia kwa makombora ya masafa ya mbali makazi ya raia katika mji wa Tehran. Mashambulio hayo dhidi ya makazi ya raia mjini Tehran katika miji mingine ya Iran yalidumu kwa muda wa mwezi mmoja ambapo mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa. Sababu ya kutekelezwa mashambulio hayo dhidi ya makazi ya raia ilikuwa ni kufidia kushindwa kwake utawala wa Saddam Hussein katika medani ya vita na Iran, na kutoa mashinikizo dhidi ya raia na viongozi wa Iran ili wakubaliane na matakwa yake ya kidhalimu na yasiyo ya kiadilifu. ***

Taswira ya mashambulio ya anga dhidi ya mji wa Tehran