Alkhamisi tarehe 5 Machi 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Rajab 1441 Hijria inayosadifiana na Machi 5 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein Bin Ali Bin Abi Twalib (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi na kuanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake, Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia na kiapo cha utiifu kwake. Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake. Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa ikimsumbua. Maadui hao wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar.

Siku kama ya leo miaka 1246 iliyopita sawa na 10 Rajab 195 Hijria, alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina, Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW. Imam Taqi Al-Jawad AS alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha AS. Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam mwema huyu, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: "Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui."

Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, sawa na tarehe 5 Machi 1827 alifariki dunia Alessandro Volta, mtaalamu wa fizikia wa Italia akiwa na umri wa miaka 83. Sambamba na kufundisha katika chuo kikuu, Volta alikuwa akifanya uhakiki na alifanikiwa kutengeneza chombo cha kupimia kiwango cha umeme Electrometre.
Miaka193 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Pierre Laplace mwanahisabati mashuhuri wa kifaransa. Alizaliwa mwaka 1749 na baada ya kuhitimu masomo yake alijishughulisha na kufundisha hisabati. Laplace alitumia sehemu kubwa ya umri wake kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na elimu za nujumu na hisabati.
Tarehe 5 Machi miaka 67 iliyopita alifariki dunia Joseph Stalin, kiongozi na dikteta wa Urusi ya zamani. Stalin alizaliwa mwaka 1879 nchini Georgia na alijiunga na mrengo wa kikomunisti baada ya kusoma fikra za mrengo huo. Joseph Stalin alipelekwa uhamishoni huko Siberia mwaka 1913 kutokana na harakati zake za kisiasa dhidi ya serikali ya wakati huo ya Urusi. Stalin alibakia huko hadi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Urusi mwaka 1917. Alipata vyeo vya ngazi za juu wakati wa uongozi wa Lenin na alishika uongozi wa nchi hiyo akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri baada ya kufariki dunia Lenin. Mwaka 1927 Stalin aliwafutilia mbali wapinzani wake ndani ya chama na kuwa kiongozi asiye na mpinzani katika Chama cha Kikomunisti. Joseph Stalin aliendelea kuwafuta na kuwaangamiza bila ya huruma wapinzani wake ndani na nje ya chama hicho.
Tarehe 5 Machi miaka 7 iliyopita alifariki dunia rais wa zamani wa Venezuela, Hugo Chavez. Chavez aliyezaliwa tarehe 28 Julai mwaka 1954 alikuwa rais wa 64 wa nchi ya Venezuela. Alitambulika kama kinara wa "Mapinduzi ya Kibolivari" na alipata umashuhuri kwa siasa zake za demokrasia ya kisoshalisti, kupinga utandawazi wa kileberali na sera za nje za Marekani na kuziunga mkono Iran na Palestina. Hugo Chavez aliaga dunia mwezi Machi mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 58 kutokana na maradhi ya saratani.
Na siku kama ya leo miaka 4 iliyopita alifariki dunia mbunifu wa E-mail yaani baruapepe, Ray Tomlinson. Tomlinson ambaye mwaka 1971 alikuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya uhakiki kama mhandisi huko Boston nchini Marekani alianzisha mfumo wa awali wa E-mail katika mtandao wa Arpanet yaani nakala ya kwanza na intaneti. Mtaalamu huyo kwa hakika alituma baruapepe ya kwanza kabisa kwa mtindo wa kisasa. Ray Tomlinson alifariki dunia katika tarehe aliyozaliwa akiwa na umri wa miaka 75 kutokana na ugonjwa wa kiharusi.