Ijumaa tarehe 6 Machi 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 11 Rajab 1441 Hijria sawa na Machi 6 mwaka 2020.
Miaka 1170 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa mjini Baghdad mtaalamu wa fasihi, lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu, Abubakar Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn al Anbari. Alijifunza elimu ya Hadithi baada ya kukamilisha masomo yake ya lugha na sayansi za Qur'ani tukufu. Ibn al Anbari alikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kuhifadhi na kushika vitu kichwani mwake. Alikwua mtu mwema na mchamungu saba na mbali na kujishughulisha na kufundisha na kuklea vizzi vya maulamaa mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya "Adabul Kaatib" na "Dhamaairul Qur'ani." Alifariki dunia mwaka 328 Hijiria akiwa na umri wa miaka 57.

Miaka 870 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa Hadithi Ibn Asakir. Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata elimu katika vituo vya kielimu vya Baghdad, Kufa, Mosul, Neishabur, Marv, Isfahan na Hamedan. Msomi huyo ameandika vitabu 134 kikiwemo kile cha "Tarikh Dimishqi."

Siku kama ya leo miaka 545 iliyopita, alizaliwa Michelangelo, mchoraji na mhunzi wa masanamu wa Italia katika mjini Caprese. Licha ya upinzani mkubwa wa baba yake dhidi ya sanaa hiyo ya uhunzi na uchoraji, Michelangelo alijiendeleza katika taaluma hiyo na kupata umahiri mkubwa. Uhodari wake ulionekana miaka michache baadaye ambapo alifanikiwa kuchonga masanamu mengi ya kuvutia. Michelangelo, alitokea kuwa mhunzi hodari wa karne ya 16 Miladia. Mwaka 1505, wakazi wa mji wa Roma walimwalika Michelangelo, ili aende kuwachongea sanamu la papa kwenye kaburi lake. Baadaye papa wa wakati huo, alimtaka mtaalamu huyo kupamba paa la kanisa la Sistine, kazi iliyoanza hapo mwaka 1508 na kumalizika mwaka 1512. Mbali na hayo, Michelangelo alichonga sanamu kubwa la Nabii Issa (as), ambalo lipo mjini Roma hadi leo.
Siku kama ya leo miaka 468 iliyopita yaani tarehe 6 Machi 1552, vilimalizika vita vikubwa vya pili kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ujerumani, kwa kushindwa Waprotestanti. Vita hivyo vilipiganwa nchini Austria. Sababu ya vita hivyo zilikuwa za kimadhehebu na vilianza baada ya Martin Luther kuanzisha madhehebu ya Kiprotestanti katika dini ya Kikristo.
Miaka 120 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia mvumbuzi wa Kijerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64. Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi.
Siku kama ya leo, miaka 83 iliyopita, alizaliwa, Valentina Tereshkova, mwanamke wa kwanza mwanaanga wa dunia. Akiwa kijana na baada ya kushiriki katika mashindano ya kuruka kwa mwavuli, Tereshkova aliibuka mshindi na hivyo kufikia daraja la ukapteni katika kikosi cha anga cha jeshi la Urusi ya zamani. Ni baada ya hapo ndipo akajifunza urubani wa ndege. Hatimaye tarehe 16 mwezi Juni, mwaka 1963 na akiwa na umri wa miaka 22, aliweka rekodi ya dunia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mwanaanga, baada ya kuanza safari ya mwezini na chombo cha Vostok 6.
Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, aliuawa Ali Razmara, Waziri Mkuu wa Iran aliyekuwa kibaraka wa Uingereza. Razmara aliyekuwa jenerali wa jeshi katika utawala wa kifalme aliuawa na mwanamapinduzi wa Kiislamu aliyejulikana kwa jina la Khalil Tahmasbi. Usaliti na uovu wa wazi wa Ali Razmara katika siasa za kuiongoza nchi, ulizusha upinzani mkubwa wa wananchi dhidi ya Waziri Mkuu huyo na kutayarisha mazingira ya kuangamizwa kwake.
Tarehe 6 Machi miaka 63 iliyopita, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah. Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo.