Mar 06, 2020 22:57 UTC
  • Jumamosi, Machi 7, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Rajab 1441 Hijria, sawa na tarehe 7 Machi 2020 Miladia.

Tarehe 12 Rajab miaka 1409 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume SAW na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi. Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka. Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.***

Abbas bin Abdul Muttalib

 

Miaka 1235 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Hudheifa mpokezi wa hadithi, habari za kihistoria na mwandishi mkubwa wa visa vya Mitume. Kwa muda fulani aliishi katika miji ya Makka na Madina na kujishughulisha na masomo ya hadithi. Abu Hudheifa alikuwa mpokezi wa hadithi mwenye itibari kubwa. Miongoni mwa vitabu vyake muhimu ni pamoja na kile cha "Al Mubtada" kinachohusu uumbwaji wa mwanadamu na visa vya Mitume. Kitabu chake kingine ni kile kinachohusu uchambuzi wa hadithi ya Imam Swadiq (as) kuhusu Mi'raji ya Mtume Mtukufu (saw). ***

Abu Hudheifa

 

Katika siku kama ya leo miaka 746 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano Thomas Aquinas. Alizaliwa mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo hadi Chuo Kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu. Aquinas kama alivyokuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya viwili hivyo inataka kujua hakika na ukweli. Itikadi za Aquinas na misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu. ***

Thomas Aquinas

 

Siku kama ya leo miaka 255 iliyopita,  alizaliwa Nicephore Niepce mwanakemia wa Kifaransa na mmoja wa waasisi wa fani ya upigaji picha. Niepce alikuwa mtu wa kwanza aliyefanikiwa kupiga picha ya kwanza duniani. Baada ya hapo, Nicephore alitengeneza kamera ya kupiga picha kwa kushirikiana na marafiki zake. Mwanakemia huyo wa Ufaransa aliaga dunia mwaka 1833. ***

Nicephore Niepce

 

Miaka 232 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 12 Rajab, utawala wa ukoo wa Zandiye nchini Iran ulifikia tamati baada ya kuaga dunia Lotfi Ali Khan  Zand. Jiwe la msingi la utawala wa ukoo wa Zandiye liliwekwa na Mohammed Karim Khan Zand mwaka 1165 Hijria na binafsi alikuwa akitambua kama mwakilishi wa wananchi na alifanya hima ili watu waishi katika utulivu. Hata hivyo aliyekuja kumrithi alijihusisha zaidi na mizozo kwa ajili ya madaraka. Ndio maana utawala wa Zandiye ukadhoofika na mahasimu wake akiwemo Agha Muhammad Khan Qajar wakapata nguvu. Lotfi Ali Khan Zand aliyekuwa mtawala wa mwisho wa ukoo wa Zandiye, alikuwa kijana shujaa na mkweli, hata hivyo kutokana na kutokuwa na tajiriba ya kutosha alishindwa na Agha Muhammad Khan na aliuawa baada ya kuteswa sana. ***

Lotfi Ali Khan  Zand

 

Na katika siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ujerumani ya Kinazi vilifanya mashamulizi ya kwanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Wanajeshi wa Ujerumani walipuuza makubaliano ya Warsaw na Locarno kwa amri ya Adolph Hitler na hivyo kuingia eneo la Ranani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Locarno na Warsaw, eneo la Ranani lililokuwa likigombaniwa kati ya Ufaransa na Ujerumani lilitangazwa kuwa eneo lisiloegamea upande wowote. Hata hivyo jeshi la Ujerumani liliamua kuliteka na kulikalia kwa mabavu eneo hilo katika siku kama hii ya leo. ***

Adolph Hitler