Jumanne tarehe 10 Machi mwaka 2020
Leo ni Jumanne tarehe 15 Rajab mwaka 1441 Hijria sawa na mwezi Machi mwaka 2020.
Tarehe 15 Rajab miaka 1446 iliyopita kundi la kwanza la Waislamu lilianza safari ya kuondoka Makka na kuhamia Uhabeshi barani Afrika. Hijra hiyo iliyokuwa na taathira kubwa katika harakati za Uislamu ilifanyika miaka 8 kabla ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Baada ya kushadidi mashaka ya Waislamu waliokuwa wakiteswa na kusumbuliwa na washirikina wa Makka, Mtume Muhammad (saw) aliwaamuru baadhi ya maswahaba zake waelekee katika ardhi ya Uhabeshi barani Afrika kwa ajili ya kujilinda na adha na mateso ya washirikina. Kundi hilo la Waislamu lililojumuisha wanaume 11 na wanawake 4 likiongozwa na Uthman bin Madh'un, lilihamia Uhabeshi na kutayarisha uwanja na mazingira mazuri ya Hijra ya pili ya Waislamu kuelekea katika ardhi hiyo ya Afrika. Kundi hilo la pili liliongozwa na binamu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ja'far bin Abi Twalib. Hijra hizo mbili zilikuwa na mchango mkubwa wa kueneza zaidi dini ya Uislamu barani Afrika.

Miaka 1439 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, Kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas. Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas.
Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Bibi Zaynab (AS) mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi. Bibi Zaynab AS alizaliwa mwaka wa 6 Hijiria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake Imam Ali AS na mama yake Bibi Fatimat Zahra AS. Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab AS alishiriki katika tukio la Karbala pamoja na kaka yake Imam Hussein AS na watu wengine wa familia ya Mtume SAW. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake.

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita mwafaka na tarehe 15 Rajab mwaka 60 Hijria, alifariki dunia Muawiyah bin Abu Sufiyan, adui mkubwa wa Ahlibaiti wa Mtume Muhammad (saw) na mwasisi wa utawala wa Bani Umayyah. Muawiyah alizaliwa miaka 15 kabla ya kuhama Mtume SAW kutoka Makka na kuelekea Madina, na alisilimu wakati wa kukombolewa Makka na jeshi la Kiislamu katika mwaka wa 8 Hijria. Muawiyah alishika Uliwali wa Sham wakati wa Ukhalifa wa Omar bin Khattab na wakati wa uongozi wa Imam Ali bin Abi Twalib (A.S) alianzisha vita vya Siffin kwa kisingizio cha kulipiza kisasi cha kuuawa Othman bin A'ffan.

Tarehe 10 Machi miaka 144 iliyopita mvumbuzi wa Kimarekani Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano.
Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka. Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell.
Tarehe 10 Machi siku kama ya leo miaka 124 iliyopita jeshi la Italia lilishindwa vibaya katika jaribio lake la kutaka kuivamia na kuikalia kwa amabavu Uhabeshi au Ethiopia ya sasa. Lengo kuu la shambulizi hilo la Italia lilikuwa ni kuiungunisha Ethiopia na makoloni mengine mawili ya nchi hiyo yaani Somalia na Eritrea. Katika vita hivyo jeshi la Italia lilipata kipigo na hasara kubwa ya hali na mali licha ya kuwa na silaha za kisasa na kulazimika kurudi nyuma.
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo. Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Haj Hussein Khadimi alizaliwa mjini Isfahani, Iran mwaka 1280 Hijiria Shamsia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Naini, Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Sheikh Muhammad Jawad Balaghi. Akiwa na umri wa miaka 26 alifikia daraja ya ijtihadi ambapo baada ya kurejea mjini Isfahani alijikita na shughuli ya ufundishaji sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi ambapo alikuwa na wanafunzi wengi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake kutovaa hijabu Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran.