Jumamosi, 21 Machi, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 26 Rajab 1441 Hijria sawa na tarehe 21 Machi 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 2193 iliyopita, Bunge la kwanza la Iran lililokuwa likijulikana kwa jina la Mahestan liliasisiwa. Wajumbe wa Bunge hilo lililoasisiwa katika zama za Mehrdad wa Kwanza mfalme wa ukoo wa Ashkanian walikuwa ni wana wafalme na shakhsia wakubwa wa Iran. Miongoni mwa yaliyokuwa mamlaka ya Bunge la Mahestan ni kumchagua mfalme na kumuondoa madarakani endapo atakumbwa na maradhi mabaya, kuwa kichaa, kushindwa kufanya kazi au kuisaliti nchi. Aidha Bunge hilo lilikuwa na jukumu la kutangaza vita au kupendekeza amani na sulhu. ***
Miaka 1444 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume SAW katika mji wa Makka. Baada ya kufariki Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad SAW, Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume na akawa bega kwa bega na Mtume katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad SAW, Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na alisimama imara kukabiliana na washirikina wa Kiqureishi. Baada ya kufariki dunia Abu Talib, washirikina walizidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume SAW kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo aliondoka Makka na kuhamia Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu. ***

Katika siku kama ya leo miaka 883 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Ibn Dobaysi, mwanahistoria, mpokezi wa hadithi na fakihi mahiri wa Kiislamu alizaliwa huko Iraq. Ibn Dobaysi alisoma masomo ya dini na kufanikiwa kuwa mahiri na kisha kuanza kufundisha na kuandika vitabu. Alikuwa na kipaji cha hali ya juu katika kuhifadhi mambo na aghlabu ya yale aliyokuwa akiyafundisha alikuwa ameyahifadhi. ***
Siku kama ya leo miaka 252 iliyopita inayosadifiana na 21 Machi 1768, alizaliwa Joseph Baron Fourier mwanahisabati na mwanafizikia mashuhuri wa Ufaransa. Baron Fourier alikuwa ni miongoni mwa wahadhiri wa mwanzoni kabisa waliofundisha somo la hesabati mara baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Paris.***
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku ya mauaji ya umati dhidi ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini yaliyotokea mwaka 1960 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kufuta Ubaguzi wa Rangi". Waafrika weusi wapatao 69 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa katika siku kama ya leo, baada ya askari makaburu kuwafyatulia risasi watu hao waliokuwa wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga siasa za ubaguzi wa rangi. Japokuwa sera za ubaguzi wa rangi zimefutwa nchini Afrika Kusini lakini ubaguzi na ukosefu wa usawa vingali vinashuhudiwa kwa sura mbalimbali katika maeneo tofauti ya dunia na hivyo kunahisika haja ya kusimama na kukabiliana na miamala hii isiyo ya kibinadamu.***
Katika siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, kulitokea mapigano makubwa kati ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Karama ulioko Jordan. Kwa uchache wanajeshi 1,230 wa Kizayuni waliangamizwa na makumi ya vifaru kutekelezwa au kuchukuliwa ngawira na wanamapambano wa Kipalestina kwenye mapigano hayo. Harakati ya PLO ilianza kupoteza hadhi yake ya kimapambano baada ya kulegeza misimamo yake ya kimapinduzi mwaka 1991 na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani na utawala ghasibu wa Israel; mazungumzo ambayo hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina. ***
Miaka 30 iliyopita katika nchi ya Namibia ilipata uhuru kutoka kwa Afrika Kusini. Mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni wa Kijerumani, Uingereza na Ureno walianza kuvutana kwa minajili ya kudhibiti na kupora utajiri na maliasili za Namibia. Uhuru wa Namibia ulipatikana kutokana na mapambano ya harakati ya SWAPO chini ya uongozi wa Sam Nujoma. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya 'Fat-hul Mubiin' ya wapiganaji shujaa wa Kiislamu huko kusini magharibi mwa Iran kwa shabaha ya kuyarejesha nyuma majeshi vamizi ya Iraq. Kwenye operesheni hiyo iliyopelekea kukombolewa miji ya Dezful, Andimeshk, Shush na mamia ya vijiji vya eneo hilo, wanajeshi wasiopungua elfu 25 wa Iraq waliuawa na wengine elfu 15 kukamatwa mateka. ***
