Jumanne tarehe 24 Machi 2020
Leo ni tarehe 29 Rajab 1441 Hijria sawa na Machi 24 mwaka 2020.
Siku kama ya leo, miaka 1165 iliyopita, alifariki dunia Abdullah bin Muslim Dinuri, maarufu kwa jina la Ibn Qutaybah akiwa na umri wa miaka 63. Ibn Qutayba alizaliwa mjini Kufah, Iraq na kushika hatamu za ukadhi huko mjini Dinuri, magharibi mwa Iran. Alitabahari katika Qur’ani, Hadithi, mashairi na fasihi. Alimu huyo aliandiandika vitabu mbalimbali katika elimu za Kiislamu maarufu zaidi vikiwa ni “Ta’awiilu Mushkili-Qur’ani”, “Tafsiru Ghariibul-Qur’an”, “Uyunul-Akhbaar”, “Maani ash-Shi’ir” na “Gharibul- Hadith.”
Miaka 114 iliyopita katika siku kama leo, alifariki dunia mwandishi wa hadithi wa Kifaransa Jules Verne akiwa na umri wa miaka 77. Verne alizaliwa Februari mwaka 1828 na alifanikiwa kuandika vitabu vingi na vya kuvutia vya hadithi ambapo ndani yake alielezea utabiri wake kuhusu ustawi wa sayansi ya mwanadamu. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na vitabu alivyoviita Twenty Thousand Leagues Under the Sea, A Journey to the Center of the Earth na Around the World in Eighty Days. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, filamu mbalimbali zenye kutoa mafunzo kwa watoto na vijana zilitengenezwa kwa mujibu wa baadhi ya hadithi hizo za Jules Verne.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, msikiti mkuu wa mji wa Ganja ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Azerbaijan ulikarabatiwa na kufunguliwa upya baada ya kufungwa kwa miaka 70. Msikiti huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1920 na kufunguliwa tena katika muongo wa 80 katika hafla iliyofanyika sambamba na kuswaliwa Swala ya jamaa. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, makumi ya misikiti ilikarabatiwa na kutumiwa na Waislamu kufuatia matukio ya kisiasa yaliyotokea Urusi ya zamani na katika jamhuri zake na pia kutokana na matakwa ya Waislamu wote wa Jamhuri ya Azerbaijan.
Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na kifua kikuu au Tuberculosis. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 daktari Robert Koch daktari na mtafiti wa Kijerumani alieleza uvumbuzi wake wa ugonjwa wa kifua kikuu katika mkutano uliofanyika Berlin na kwa mnasaba huo siku hii ya tarehe 24 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kifua Kikuu.
