Mar 29, 2020 22:00 UTC
  • Jumatatu tarehe 30 Machi 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 5 Shaaban 1441 Hijria sawa na tarehe 30 Machi mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kuswali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa shahidi baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah, Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

Siku kama ya leo miaka 1128 iliyopita alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadaye Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi.

Muhammad bin Zakaria Razi

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, Russia iliiuzia Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo. Alaska ina ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja na nusu ni jimbo la 49 la Marekani. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, hususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki.

Tarehe 30 Machi miaka 44 iliyopita, maandamano makubwa yaliyopewa jina la "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, tarehe 18 Oktoba mwaka 1975, mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walielezea kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo. Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa.

Siku ya Ardhi