Jumanne, tarehe 31 Machi, 2020
Leo ni Jumanne tarehe 6 Shaaban mwaka 1441 Hijria sawa na 31 Machi mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1283 iliyopita, Zaid bin Ali bin Hussein, mjukuu wa Imam wa Tatu wa Waislamu wa Kishia, alipeperusha bendera ya harakati yake huko mjini Kufa, Iraq wakati wa utawala wa Bani Umayyah. Mapambano ya Zaid ambayo wafuasi wake walitambuliwa kwa jina la Zaidiyyah, yaliendelea kwa muda miaka miwili na mwaka 739 Miladia, aliuawa shahidi na Yusuf Ibn Omar Thaqafi, mmoja wa watawala wa Bani Umayyah. Kufuatia matukio hayo, baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo (Zaid bin Ali) ambao hawakuwa Wairani walihamia nchini Yemen na tangu wakati huo Yemen inajulikana kama kituo kikuu cha Waislamu wa Shia Zaidiyyah. Hii leo nusu ya jamii ya Wayemen inaundwa na Mashia Zaidiyyah, Shia Ithna Ashariyyah na Shia Ismailia ambao wanapatikana zaidi katika mMaeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Miaka 424 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alipata daraja ya uhadhiri wa chuo kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa ni elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika taaluma nyinginezo. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo, Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuriwa kwa bomu, ikiwa ni katika mwendelezo wa mauaji ya umati yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya Wapalestina. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni waliokuwa na silaha na kuuwa Wapalestina 24. Wapalestina wengine 61 walijeruhiwa.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi, faqihi, mfasiri wa Qur'an Tukufu na hatibu mkubwa wa Iran. Ayatullah Mirza Abul-Fadhl Zahidi alizaliwa mwaka 1309 Hijiria, mjini Qum na katika familia ya elimu na maarifa ya dini. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alijiunga na masomo ya hawza kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Ayatullah Mirza Abul-Qasim Kabir Qumi, Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi, huku akisoma pia elimu ya falsafa na theolojia kwa Ayatullah Mirza Ali Akbar Mudares Yazdi ambapo alifanikiwa kufikia ngazi ya juu ya kielimu. Alikuwa miongoni mwa shakhsia waliochangia katika uhamisho wa Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi kutoka mjini Arak kwenda mjini Qum na hatimaye kuasisiwa hawza ya kielimu mjini hapo. Mbali na kubobea katika utafiti na kujibu shubuha mbalimbali za dini nyingine, alikuwa mjuzi katika masuala ya historia na jografia ya dini mbalimbali ambapo alitoa nadharia katika uwanja huo. Aidha maulama mbalimbali na maraaji walikuwa wakiheshimu nadharia zake hususan katika uga wa fiqhi huku Imamu Khomein (MA) akimpa lakabu ya 'Sheikh al-Twaifa'. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Risaalatu al-Dharar' 'Mantwiqul Hussein' na 'Maqswadul-Hussein.'
Tarehe 12 Farvardin miaka 41 iliyopita baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kushiriki kwa wingi wananchi katika kura ya maoni, taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kihistoria wa kupasisha mfumo wa utawala wa Kiislamu hapa nchini. Zaidi ya asilimia 98 ya walioshiriki waliupigia kura ya ndiyo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na tarehe 12 Farvardnin kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Jamhuri ya Kiislamu.
Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na serikali ya Cairo. Nchi za Kiarabu zilichukua msimamo huo mkali baada ya rais wa zamani wa Misri Anwar Sadat kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.