Alkhamisi tarehe Pili Aprili 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Shaaban 1441 Hijria sawa na Aprili Pili mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 879 iliyopita alizaliwa Ibn Rumiyya mpokezi wa hadithi, mtaalamu wa mimea na dawa wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Rumiyya alijifunza hadithi kutoka kwa wasomi na wapokezi hadithi wakubwa wa zama hizo na kujifunza elimu ya utaalamu wa mimea sambamba na elimu ya dini. Akiwa Andalusia, Ibn Rumiyya alianza kuchunguza na kutambua sifa za mitishamba na baadae alifanya safari katika nchi mbalimbali kama Misri, Iraq na Hijaz. Alijishughulisha na masuala ya utafiti wa mitishamba akiwa huko bila kusahau na kujifunza hadithi. Ibn Rumiyya aliandika vitabu vingi kuhusu mitishamba, fiqih na hadithi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vitabu hivyo vimepotea.

Katika siku kama ya leo miaka 215 iliyopita, alizaliwa huko nchini Denmark, Hans Christian Andersen malenga, mwandishi na msimulizi wa visa maarufu vya watoto. Andersen ambaye alikuwa mtoto wa bwana mmoja maskini na fundi viatu, alihamia Copenhagen mji mkuu wa Denmark na kuanza kucheza michezo ya kuigiza. Baada ya muda, Hans Andersen alianza kutunga visa na kuwa mashuhuri baada ya kuandika kitabu chake cha kwanza cha hadithi alichokipa jina la "Fairy Tales, Told for Children" mnamo mwaka 1838 Miladia. Siku ya kuzaliwa mwandishi huyo pia inatambuliwa kama Siku ya Kimataifa ya Kitabu cha Mtoto.
Miaka 36 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya jeshi la majini la Argentina vilivamia visiwa vya Falkland na kuvitwaa visiwa hivyo vya kiistratejia vilivyoko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Visiwa vya Falkland ambavyo kwa lugha ya Kiargentina vinaitwa Malvinas, viligunduliwa katika karne ya 16 Miladia na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza mwaka 1832.

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, aliaga dunia Papa John Paul II aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Papa John Paul II alizaliwa mwaka 1920 huko Poland na kufikia daraja ya uchungaji baada ya kuhitimu masomo ya dini. Mwaka 1964 Papa John Paul alikuwa askofu wa mji wa Kraku huko Poland na miaka mitatu baadaye akawa Kadinali. Hatimaye mwaka 1978 John Paul wa Pili aliteuliwa kushika wadhifa wa ngazi ya juu zaidi wa kanisa Katoliki, yaani Papa. Papa John Paul wa Pili alikuwa mfuasi wa mazungumzo baina ya dini mbalimbali hususan kati ya Uislamu na Ukristo. Alikuwa akipinga vikali utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja na ufisadi wa kimaadili kwa ujumla uliotanda katika ulimwengu wa Magharibi. Aidha alikosoa vikali mashambulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq.