Ijumaa tarehe 3 Aprili 2020
Leo ni tarehe 9 Shaaban 1441 Hijria sawa na Aprili 3 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 960 iliyopita aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo.

Siku kama ya leo miaka 864 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Shaaban mwaka 577 aliaga dunia Abul Barakat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa lakabu ya Ibn Anbari fakihi na mtaalamu wa lugha wa mjini Baghdad. Alihitimu masomo yake katika skuli mashuhuri ya Nidhamiya mjini Baghdad na kutokana na kufaulu vizuri masomo yake na maarifa mengi aliyokuwa nao, alianza kufundisha katika skuli hiyo. Ibn Anbari ameandika vitabu na makala nyingi za kielimu. Kitabu cha al-Asrar al-Arabiyah ni moja ya athari mashuhuri ya alimu huyo.

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita Otto Von Bismarck mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na Kansela wa Ujerumani, alivuliwa madaraka na Kaiser Wilhelm II aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Ujerumani. Licha ya kuondolewa madarakani, aliendelea kubaki kwenye wadhifa huo kwa muda mchache, lakini baada ya kushadidi hitilafu kati yake na Mfalme Wilhelm II, Bismarck alilazimika kujiuzulu. Bismarck alifariki dunia mwaka 1898.
Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Aprili 1941, mji wa Baghdad ulikombolewa na Rashid A'li Gilani kiongozi wa mrengo uliokuwa ukiwapinga Waingereza, baada ya kujiri mapigano kati ya wazalendo wenye uchungu wa nchi yao dhidi ya serikali ya London. Gilani alikuwa akiungwa mkono na Ujerumani na kutokana na kutopata misaada kwa wakati mwafaka, vikosi vya Uingereza vilifanikiwa kuwakandamiza wafuasi wa wake. Baada ya tukio hilo serikali ya Iraq ilijiunga na nchi waitifaki katika Vita vya Pili ya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, yaani sawa na tarehe 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina. Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuzima Intifadha ya wananchi wa Palestina. Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi.