Jumapili Aprili 5
Leo ni Jumapili tarehe 11 Shaban 1441 Hijria, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1408 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, maarufu kwa jina la Ali Akbar, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake Mtume Mtukufu (saw), alinufaika sana na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake Imam Ali (as) na baba yake Imam Hussein (as). Mtukufu Ali bin Hussein, alikuwa maarufu kwa jina la Ali Akbar yaani Ali mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali. Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma na uasi wa utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo inatambiliwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Vijana.

Siku kama ya leo miaka 912 iliyopita alifariki dunia, Sanai Ghaznawi Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran mjini Ghaznen. Alizaliwa mwaka 467 Hijiria, na akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi ambapo pia ndani yake ameweka wazi fikra za kiakhlaqi na irfani za malenga. Aidha vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.
Siku kama ya leo miaka 435 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Haarlem nchini Uholanzi, ambacho kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo. Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Uhispania 1609.
Katika siku kama ya leo miaka 371 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Shaaban 1070 Hijria, Mohammad Taqi Majlisi maarufu kama Majlisi wa Kwanza, msomi na Arif mkubwa Muirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1003 Hijria Qamari katika mji wa Isfahan ambao zama hizo ulikuwa mji mkuu wa silsila ya watawala wa Safavi. Alizaliwa wakati Iran ilikuwa ikishuhudia ustawi mkubwa wa kiutamaduni na kielimu. Familia ya Allamah Majlisi ilikuwa ya wasomi na wanazuoni kiasi kwamba alipata sehemu ya masomo yake kutoka kwa baba yake na jamaa zake wengine katika familia. Baada ya kujifunza fiqhi, itikadi na tafsiri katika darasa la Sheikh Bahai, alipata umashuhuri kama alim na arif mkubwa. Alikwea daraja la juu la masomo baada ya kutembelea mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Baada ya kurejea Isfahan alijishughulisha kufunza na kutambulika kwa umahiri wake katika fiqhi, hadithi, tafsiri na itikadi.
Miaka 226 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Georges Danton, aliyekuwa miongoni mwa vinara wa mapinduzi ya Ufaransa. Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mahiri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja wa vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kumtia mbaroni na hatimaye kumuua.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani, mmoja wa maulama wachaji-Mungu wakubwa na mwanamapambano. Alizaliwa mwaka 1262 Hijiri mjini Isfahan, Iran. Baba na babu yake, walikuwa kati ya maulama wakubwa wa eneo ambapo naye pia alipata kusoma kutoka kwao elimu mbalimbali. Baada ya Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani kusoma baadhi ya masomo ya kidini kutoka kwa baba yake (yaani Muhammad Baqir Agha Najafi) alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo mjini hapo. Miaka mitano baadaye alirejea mjini Isfahan na kuwa mmoja wa maraajii wakubwa wa mji huo. Aidha mbali na masuala ya kidini, Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani alikuwa mwanaharakati mzuri wa masuala ya kisiasa. Katika uwanja huo, msomi huyo alipambana vikali na upotoshaji wa kifikra na kiutamaduni na kadhalika ufisadi wa watawala dhalimu wa wakati huo. Wakati huo huo aliongoza harakati za kimapambano dhidi ya ukoloni wa kigeni hususan Uingereza. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Fiqhul-Imaamiyyah' 'Bahth Fii Wilaayati Haakimul-Faqih' na 'Dalaailul-Ahkam.'
Na siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Majeshi ya utawala ghasibu wa Israel, siku ya tarehe 4 Aprili, yaliwaua watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni.