Jumatano tarehe 8 Aprili mwaka 2020
Leo ni Jumatano tarehe 14 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprili 8 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 802 iliyopita alifariki dunia Ibn Yunus, fakihi, tabibu na mwanahesabati mashuhuri wa Kiislamu. Alijufunza masomo ya kawaida ya zama zake kutoka kwa baba yake na wasomi wengine wa wakati huo. Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu baada ya kuhitimu masomo yake, alifundisha katika shule na vyuo kadhaa mjini Cairo Misri pamoja na kuandika vitabu kuhusiana na masuala tofauti ya kielimu. Mbali na taaluma za fik'hi, tiba na hesabati alikuwa na ujuzi mkubwa pia katika uwanja wa muziki. Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo wa Kiislamu ni kitabu kinachoitwa al-Asraar as-Sultaniyya kinachozungumzia masuala ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita inayosadifiana na tarehe 8 Aprili mwaka 1859, alizaliwa Edmund Husserl, msomi wa hisabati na falsafa wa nchini Austria. Husserl alielekea Ujerumani kwa ajili ya kujiendeleza kielimu ambapo akiwa huko alifanikiwa kufikia daraja ya Uprofesa. Kadhalika Edmund Husserl alifanya utafiti mwingi kuhusiana na elimu ya falsafa. Husserl alitambuliwa pia kuwa mwasisi wa kanuni ya Phenomenology katika falsafa, ambayo ilikuwa na taathira kubwa kwa wanafalsafa wa Kimagharibi. Aidha aliamini kwamba, lazima falsafa iambatane na hisabati, kama ambavyo aliamini kuwa dunia lazima iwe nzuri na ya kuvutia. Ameacha athari mbalimbali ikiwemo 'Falsafa ya Hisabati' 'Uchunguzi wa Kimantiki' na vitabu vingine.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliishambulia shule ya msingi ya Bahrul Baqar iliyoko umbali wa kilomita 80 Kaskazini mwa mji wa Cairo. Katika mashambulizi hayo ya kutisha watoto 46 waliokuwa wakisoma shuleni hapo waliuawa. Mashambulizi hayo ya kikatili, yaliibua hasira ya watu katika nchi mbalimbali duniani. Inasemekana kuwa, kwa muda wa miezi mitatu ya awali ya mwaka 1970 ndege za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia maeneo ya kiraia huko kaskazini mashariki mwa Misri. Tarehe 12 mwezi Februari mwaka huohuo Wazayuni pia walikishambulia kiwanda kimoja katika eneo hilo na kuua pamoja na kuwajeruhi wafanyakazi 168. Kadhalika Wazayuni waliwaua watu 12 katika mashambulizi dhidi ya mji wa al-Mansura ulio kaskazini mashariki mwa nchi hiyo tarehe 31 mwezi Machi mwaka huohuo wa 1970.Jumatano tarehe 8 Aprili 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita sawa na tarehe 8 Aprili 1980, utawala wa Baathi nchini Iraq uliwaua Shahidi Sayyid Muhammad Baqir-Sadr na dada yake, Bintul Huda. Sayyid Sadr alijifunza Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za kidini akiwa mdogo na kupata daraja ya ijtihadi akiwa kijana. Alikuwa mmoja wa walimu wakubwa wa chuo cha kidini mjini Najaf, Iraq kiasi kwamba nadharia zake katika elimu ya usulu fiqhi zilipewa umuhimu mkubwa na wasomi wengine wa Kiislamu. Msomi huyu aliyekuwa na uelewa na uwezo wa hali ya juu wa kielimu, aliuarifisha Uislamu kwa njia sahihi. Kwa kipindi kifupi Ayatullah Sadr aligeuka na kuwa kiongozi wa kifikra na kisiasa wa wananchi wa Iraq na kuyapa mwelekeo mpya mapambano ya wananchi wa nchi hiyo. Baada ya muda fulani utawala wa nchi hiyo ambao ulihisi hatari kutokana na harakati za Ayatullahi Sadr hivyo ulimtia mbaroni na kisha kumuua shahidi mwanazuoni huyo mashuhuri pamoja na dada yake, licha ya malalamiko makubwa ya maulama na wananchi Waislamu wa Iraq. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu cha "Uchumi Wetu", "Hamasa ya Nuru", "Falsafa Yetu", "Mwanadamu wa Leo na Matatizo ya Kijamii", na "Ukhalifa wa Mwanadamu na Ushuhuda wa Mitume".
Katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran iliingia katika kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinapinga vikali miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran kutokana na sera zao za kindumakuwili na za kibaguzi.

Na miaka 7 iliyopita katika siku kama ya leo Margaret Hilda Thatcher, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza alifariki dunia. Margaret Thatcher alikuwa mwanachama wa Chama cha Wahafidhina nchini Uingereza ambapo mwaka 1975 alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama hicho. Mwaka 1990 alikuwa kiongozi wa Chama cha Wahafidhina nchini Uingereza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Thatcher ndiye mwanamke wa kwanza wa Uingereza kushikilia uongozi wa chama na Uwaziri Mkuu kwa pamoja.