Jumamosi, 11 Aprili, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 17 Shaaban 1441 Hijria mwafaka na tarehe 11 Aprili mwaka 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre. Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi dawa na vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto. Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali. ***

Miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sheikh Hassanali Isfahani, arif, msomi na mwanazuoni aliyekuwa amebobea katika taaluma ya fikihi. Alizaliwa mwaka 1279 Hijria katika mji wa Isfahan katikati mwa Iran na akaanza mapema mno kusoma elimu mbalimbali kama fikihi, Usul, mantiki na falsafa. Ayatullah Isfahani akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu alielekea Najaf Iraq na baadaye Mash’had Iran na kubakia huko hadi mwisho wa umri wake. Ayatullah Isfahani alikuwa amebobea pia katika elimu za hisabati, nujumu na tiba. Hata hivyo alikuwa mashuhuri zaidi katika baadhi ya elimu kama irfan na akhlaq. ***
Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, alliaga dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania. Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia. Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Muhsin Saba mwalimu na mwandishi wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi katika shule ya Darul Funun alielekea nchini Ufaransa. Alirejea nchini Iran baada ya kupata shahada ya uzamivu (PhD) na kuanza kufundisha. Dakta Muhsin Saba aliasisi Kundi la Taifa la Utambuzi wa Vitabu. Aidha hakuwa nyuma pia katika kutunga na kuandika vitabu. ***