Apr 12, 2020 04:25 UTC
  • Jumapili Aprili-12

Leo ni Jumapili, tarehe 18 Sha’ban mwaka 1441 Hijria, sawa na tarehe 12 Aprili, 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1120 iliyopita, sawa na tarehe 18 Sha’ban mwaka 321 Hijiria, alifariki dunia Ibn Dorayd, mtaalamu wa lugha, mwanafasihi na malenga wa Kiarabu. Ibn Dorayd alikuwa mtaalamu, mwenye tabia njema na msamehevu sambamba na kuwa na uwezo mkubwa wa kumbukumbu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na kitabu kinachoitwa "Al-Ishtiqaq" ambacho kimeandikwa kwa mpangilio wa herufi za Kiarabu. Vilevile ameandika diwani na tungo za mashairi.

Ibn Dorayd

Siku kama ya leo, miaka 1115 iliyopita, sawa na tarehe 18 Sha’ban mwaka 326 Hijiria, alifariki dunia Abul-Qasim Hussein bin Ruh Nubakhti, naibu wa tatu wa Imam Mahdi (as). Abul-Qasim Hussein Nubakhti alikuwa, mtaalamu mkubwa raia wa Iran aliyetabahari katika elimu ya hadithi, fiqihi huku akibobea pia katika elimu ya theolojia. Alipata umashuhuri mkubwa baina ya Waislamu wa Kishia mjini Baghdad, Iraq katika zama za uhai wake. Aidha alim huyo alifahamika pia kwa jina la Aal Nubakhti. Mwaka 305 na 326 Hujiria, Nubakhti, alikuwa naibu na mwakilishi wa Imam Mahdi (as) mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw), na Waislamu wa Kishia. Imam Mahdi alighibu, baada ya watawala wa enzi hizo kutaka kumshika na kumuua, ambapo kwa amri ya Mwenyezi Mungu alienda ghaiba, ambapo atadhihiri tena wakati Mwenyezi Mungu atakapotaka.

Jaburi la Abul-Qasim Hussein bin Ruh Nubakhti.

Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1820, dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona. Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine. Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyia majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine.

Mbu wanaosababisha ugonjwa wa Malaria

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1823, alizaliwa Alexandr Ostrovsky mwandishi wa tamthilia wa nchini Russia. Alihitimu masomo ya sheria katika chuo kikuu ingawa aliamua kujiunga na tasnia ya uandishi wa tamthilia na uigizaji. Karibu kila mwaka Alexandr Ostrovsky alikuwa akifanya uigizaji wa kihistoria au kuandika vichekesho ambapo alikuwa akiakisi hali halisi ya jamii. Alikuwa na taathira kubwa katika senema ya Russia. Miongoni mwa athari za mwanasanaa huyo ni pamoja na 'Binti wa Barafu', 'Msitu' 'Tufani' na 'Muhanga Mwingine.' Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1886 Miladia.

Alexandr Ostrovsky

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1867, Mutsuhito, mfalme maarufu na mwanamageuzi wa Japan aliingia madarakani nchini humo. Mfalme huyo aliingia madarakani wakati ambapo Japan ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za udhaifu katika nyuga tofauti. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mutsuhito baada ya mwaka mmoja kuingia madarakani akabuni mapinduzi ya kijamii na kuanzisha mageuzi nchini Japan. Katika uwanja huo alihamisha mji mkuu kutoka Kyoto kwenya Tokyo sambamba na kubadili katiba ya nchi hiyo. Hata kama utawala wa Mutsuhito ulifikia tamati mwaka 1912, lakini Japan iliweza kupata maendeleo licha ya kuliibuka vita baina yake na China na Russia.

Mutsuhito

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1932, mfumo wa jamhuri uliasisiwa kwa muda huko Uhispania na utawala wa kifalme ukafikia ukomo. Wananchi wa Uhispania waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri waliendesha mapambano dhidi ya utawala wa kimabavu na kidikteta wa Alphonce wa 13 Mfalme wa wakati huo wa Uhispania na kumlazimisha kujiuzulu.

Bendera ya Uhispania

Na siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1961 Miladia, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia. Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga. Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.

Yuri Gagarin