Apr 13, 2020 02:12 UTC
  • Jumatatu tarehe 13 Aprili 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 19 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprili 13 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita vita vya Bani al-Mustalaq vilipiganwa. Bani al-Mustalaq lilikuwa moja ya makabila ya Khuza'ah ambayo katika zama za kale yalikuwa yakiishi katika viunga vya mji mtakatifu wa Makka. Wazee wa makabila hayo walikuwa wakieneza ibada ya miungu na masanamu mjini humo. Baada ya Waislamu kuunda dola huko Madina, kabila la Bani al-Mustalaq ambalo lilikuwa likishikilia msimamo wake wa kuendelea kuabudu masanamu lilitangaza vita dhidi ya jeshi la Waislamu. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) akiwa na wafuasi wake waliamua kukabiliana na makafiri hao ambapo kabila la Bani Mustalaq lilishindwa vibaya katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, kulijiri tukio la umwagaji damu mkubwa katika Bustani ya Jallianwala nchini India. Mwaka 1919 na kwa lengo la kuzuia uasi na mapambano ya wananchi, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipasisha sheria iliyowapa polisi haki ya kuwatia mbaroni wanaharakati wa India bila sababu yoyote na kuwashikilia kwa muda usiojulikana. Sheria hiyo iliwakasirisha mno wananchi wa India na katika siku kama ya leo zaidi ya Wahindi elfu tano waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika Bustani ya Jallianwala katika mji wa Amritsar walimiminiwa risasi kwa amri ya kamanda mmoja wa Uingereza. Watu 1200 waliuawa na wengine 4000 kujeruhiwa katika tukio hilo. Baada ya mauaji hayo, harakati ya ukombozi wa India ikiongozwa na shujaa Mahatma Ghandhi ilipamba moto.

Mahatma Ghandhi

Tarehe 13 Aprili mwaka 1945 yaani miaka 75 iliyopita, Austria ilidhibitiwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya nchi waitifaki. Tukio hilo lilijiri katika miezi ya mwisho ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Kabla ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Austria ilikuwa nchi huru na inayojitawala. Lakini muda mchache baada ya kuanza vita hivyo, Adolph Hitler aliiunganisha ardhi ya nchi hiyo na Ujerumani na wanajeshi wa Austria wakaingia vitani kupigana upande wa Ujerumani. Baada ya Ujerumani kuondoka Austria na nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na madola waitifaki, iligawanywa katika maeneo matano ambapo kila eneo likadhibitiwa na kuendeshwa na moja ya madola hayo, huku mji mkuu Vienna ukiendeshwa kwa pamoja na madola manne. Hatimaye mwaka 1946, madola waitifaki yalitambua rasmi uhuru wa Austria ambapo baada ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya pande mbili, mwaka 1955, majeshi ya nchi waitifaki yakaondoka katika ardhi ya Austria.

Bendera ya Austria

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, shambulio la wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja lililolenga basi moja lililokuwa na Wapalestina na kuua watu 30 kati yao, lilipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Lebanon. Kufuatia mauaji hayo, Waislamu na wazalendo wa Lebanon walianzisha mapambano ya kukabiliana na Mafalanja hao. Muda mfupi baadaye harakati za wapiganaji wa Kipalestina pia ziliingia katika vita hivyo vya ndani vya Lebanon. Vita hivyo ambayo vilikuwa vikichochewa na utawala haramu wa Israel, viliisababishia hasara kubwa ya mali na roho serikali ya Beirut.

Wanamgambo wa Kikristo, Lebanon

Siku kama ya leo sawa na tarehe 25 Farvardin miaka 32 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri waziwazi kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu. Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo. Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya malengo ya kijeshi na kiraia ya Iran. Takwimu zimeonesha kwamba utawala wa Baath wa Iraq ulifanya mashambulizi 3,500 kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha vita hivyo.

Iraq ilikiri kutumia silaha za kemikali.

Katika siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, yaani tarehe 13 Aprili 2003, maandamano ya kwanza ya wananchi wa Iraq dhidi ya wavamizi baada ya miongo mitatu ya mbinyo na ukandamizaji ya utawala wa diikteta Saddam Hussein yalifanyika. Baada ya kuangushwa utawala wa Saddam na chama cha Baath Aprili 9 mwaka 2003 na kisha nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na vikosi vamizi hususan majeshi ya Marekani, maandamano ya kwanza ya wananchi ya kupinga kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchi yao yalifanyika.

Na leo tarehe 25 Farvardin kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi arif na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Fariduddin Attar Naishaburi. Attar Naishaburi alizaliwa karibu mwaka 540 Hijria na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafasfi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu ya kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantwiqut Twair."