Jumatano tarehe 15 Aprili 2020
Leo ni Jumatano tarehe 21 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprili 15 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 935 iliyopita alizaliwa Abdulkarim bin Muhammad as-Sama'ani maarufu kwa lakabu ya Tajul Islam faqih, mpokeaji hadithi na mwanahistoria mtajika wa karne ya sita Hijria huko katika mji wa Marw kusini mashariki mwa Tukimanistan ya sasa na Khurasan kubwa ya zamani. As-Sama'ani alipitisha miaka mingi ya umri wake kwa kufanya safari katika nchi mbalimbali kama vile Iran, Sham, Hijaz na nyinginezo na kunufaika na bahari kubwa ya wasomi wa kila sehemu aliyokwenda. Kitabu maarufu cha msomi Sama'aani ni kile alichokita kwa jina la " al Ansaab."

Siku kama ya leo miaka 568 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mashuhuri wa kutengeneza vinyago wa Italia Leonardo da Vinci. Alionesha kipaji kikubwa cha kuchora akiwa bado mtoto mdogo na alikweya daraja za juu katika fani hiyo haraka mno. Mwaka 1506 Miladia da Vinci alichaguliwa kuwa mchoraji wa Mfalme Luis wa 12 kisha akawa mchoraji wa Mfalme Francis wa Kwanza. Mbali na uhodari wake katika kuchora na kutengeneza vinyago, Leonardo da Vinci pia alisomea fizikia na hisabati. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni michoro ya kanisa kuu la mji wa Milan, mchoro wa picha ya "Tabasamu la Jugund," picha ya Mona Lisa na ya Karamu ya Mwisho ya Issa Masih (as). Leonardo da Vinci alifariki dunia mwaka 1519 akiwa na umri wa miaka 67.

Katika siku kama ya leo miaka 108 iliyopita meli kubwa ya abiria ya Titanic ambayo ilitambuliwa kuwa nembo ya mafanikio makubwa ya viwanda vya meli vya wakati huo iligonga mwamba wa theluji na kugharibi katika Bahari ya Atlantic, katika safari yake ya kwanza kutoka bandari ya Southampon nchini Uingereza ikielekea New York, Marekani. Zama hizo Titanic ilitambuliwa kuwa meli kubwa zaidi na ya kifahari kuliko zote duniani. Watengenezaji wa meli hiyo walikuwa akisema kuwa haiyumkini kughariki na kuzama. Wasafiri 705 tu kati ya abiria wake wote 2207 ndio waliookoa katika ajali hiyo. Ajali hiyo inatambuliwa kuwa mbaya zaidi ya baharini na iliyosababisha idadi kubwa ya vifo duniani.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, yaani sawa na tarehe 15 Aprili 1988, shirika la ujasusi la utawala bandia wa Israel MOSSAD lilimuua shahidi Khalil al Wazir maarufu kwa jina la Abu Jihad mwasisi na shakhsia nambari mbili wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO huko Tunis, Tunisia. Abu Jihad aliongozana na wenzake nchini Misri, na huko wakaamua kuanzisha harakati ya mapambano dhidi ya Wazayuni, na kuipatia jina la Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO.
Miaka 34 iliyopita katika siku kama leo, Marekani iliishambulia miji ya Tripoli na Benghazi nchini Libya. Kisingizio kilichotumiwa na Washington kufanya mashambulizi hayo ya anga ni kuwa Libya ilihusika katika mlipuko uliotokea kwenye mkahawa mmoja mjini Berlin, Ujerumani ambapo askari watatu wa Marekani waliuawa. Raia kadhaa ambao hawakuwa na hatia yoyote waliuawa katika mashambulizi hayo ya Marekani katika miji ya Tripoli na Benghazi. Mashambulizi hayo yaliamsha hasira za Waislamu na kulaaniwa vikali na jamii ya kimataifa.
Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kuanzisha Shirika la Biashara Duniani (WTO) nchini Morocco. Utangulizi wa kuasisiwa shirika hilo ulifanywa na Marekani na Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kwa msingi huo, mwaka 1947 nchi 23 zilizoendelea zilitia saini makubaliano ya kuanzisha GATT. Makubaliano hayo yalisisitiza juu ya kufanyika mazungumzo ya kupunguza ushuru wa forodha na vizuizi vya biashara huru. Baadaye jumuiya ya GATT ilibadilishwa jina na kuwa WTO na hati yake kuanza kutekelezwa Januari mwaka 1995. Hata hivyo Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeliteka shirika hilo la kibiashara duniani na kulitumia kwa faida na maslahi yao wenyewe.
