Apr 16, 2020 23:52 UTC
  • Ijumaa, tarehe 17 Aprili, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 23 Shaabani 1441 Hijria inayosadifiana na Aprii 17 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1137 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh, maarufu kwa lakabu ya Nasser Kabir, alimu na mwanamapambano mkubwa miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Alizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina, na baada ya watawala wa Bani Abbas kuwaua na kuwabaidisha watu wa familia ya Mtume SAW akiwemo Imamu Hassan Askari (as), Ali Atroosh alipelekwa mjini Samarra, kaskazini mwa mji wa Baghdad, Iraq kwa amri ya watawala hao ikiwa ni baada ya baba yake kubaidishwa mjini hapo. Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh alijifunza elimu ya dini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa msomi mkubwa huku akitabahari pia katika uwanja wa mashairi. Mbali na hayo alijihusisha na harakati za kisiasa ambapo katika kipindi cha mwamko wa Maalawi mjini Tabarestan, kaskazini mwa Iran, Atroosh alikimbilia katika eneo hilo. Baada ya kuanguka utawala huo, aliufufua huku akitawala sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini mwa Iran kwa uadilifu na usawa, sambamba na kueneza mafundisho ya dini ya Mtume Muhammad (saw). Katika harakati zake alifanikiwa kuwaingiza maelfu ya watu katika dini ya Uislamu. 'Al-Bisat' 'Tafsir al-Utrush' na 'Imamatul-Kabir ni miongoni mwa makumi ya vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo. 

Abu Muhammad Hassan Ibn Ali Atroosh,

Miaka 708 iliyopita na katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Hussein bin Abdullah Tayyebi aliyekuwa na lakabu ya Sharafuddin aliaga dunia. Alikuwa mpokezi wa hadithi na na mwanafasihi mkubwa. Abdullah Tayyebi alibobea katika elimu za fasihi ya lugha ya Kiarabu na alihesabiwa kuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika zama zake. Mwanazuoni huyo alikuwa akitilia mkazo suala la kufundisha tafsiri ya Qur'ani pamoja na Hadithi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni 'Tafsirul-Qur'an' na 'Sherh al Meshkat'.

Miaka 624 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Nuruddin Abdul-Rahman Jami, mshairi na mwanafasihi mkubwa wa Kiirani wa karne ya 9 Hijria. Alizaliwa katika mji wa Jam ulioko katika mkoa wa Khorasan kaskazini mashariki mwa Iran. Alianza kujifunza elimu mbalimbali akiwa katika rika la ujana. Alikuwa na mapenzi na itikadi thabiti na watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW. na katu hakuwahi kuwasifu wafalme na watawala. Silsilat al-Dhahab na Baharestan ni baadhi ya athari za Nuruddin Abdul Rahaman Jami.

Tarehe 17 Aprili miaka 105 iliyopita kwa mara ya kwanza kabisa duniani ilitumiwa gesi ya kubana pumzi ya wanadamu vitani. Hatua hiyo ya kinyama ilichukuliwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Ujerumani ilitumia gesi hiyo ya kubana pumzi dhidi ya askari wa Uingereza na Ufaransa na kuua askari wengi wa vikosi vya waitifaki. Wajerumani walipata ushindi katika vita hivyo vilivyokuwa mashuhuri kwa jina la Vita vya Gesi.

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, raia wa Scotland, John Logie Baird, alifanikiwa kuvumbua televisheni ambayo hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa katika upashaji habari duniani. Baird alikuwa mmoja wa wavumbuzi wakubwa wa enzi zake. Baada ya hapo mtu wa kwanza kutengeneza televisheni iliyoimarika zaidi alikuwa ni Giovanni Caselli, raia wa Italia ambaye mnamo mwaka 1862 alifanikiwa kutengeza chombo ambacho kwa kutumia mfumo wa telegrafi kiliweza kutoa ramani na picha. Televisheni ya kwanza ambayo ilionyesha picha kwa ufasaha, ilianza kutumika tarehe 17 mwezi April mwaka 1926 kwa ajili ya klabu ya kifalme nchini Uingereza. 

John Logie Baird

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mjini wa Mash'had huko kaskazini mashariki mwa Iran.  Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikuwa mwana wa marhoum Hujjatul Islam wal Muslimin Hajj Sayyid Javad Husseini Khamenei na alikuwa mtoto wa pili katika familia. Maisha ya Sayyid Javad Khamanei, sawa na ya wanazuoni wengi yalikuwa sahaji sana. Ayatullah Khamenei alipata malezi bora katika familia ya kidini na kuanza kusoma akiwa na umri wa miaka minne. Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatulla Khamenei alianza masomo  chini ya usimamizi wa mwanazuoni na marjaa maarufu Ayatullahil Udham Milani.  Sayyid Ali Khamenei alianza masomo ya dini chini ya usimamizi wa baba yake na kupiga hatua zaidi za maendeleo katika uwanja huo. Hatimaye alielekea katika mji mtakatifu wa Qum na kuendelea na masomo ya juu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kwa muda wa miaka saba. Wanazuoni kama Imam Khomein MA, Ayatullahil Udhma Burujardi na Allamah Tabatabai ni miongoni mwa wasomi ambao Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alipata elimu kutoka kwao. Katika kipindi cha ujana wake Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei alijiunga na harakati za Imam Khomein MA za kuupinga utawala wa kidikteta wa Shah. Alieneza fikra za Imam Khomein na kufichua ufisadi wa viongozi waliokuwa katika utawala wa wakati huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikamatwa na kutiwa gerezani mara kadhaa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mwanachama wa Baraza la Mapinduzi na kisha baada ya hapo, aliwahi pia kuchaguliwa kuwa mbunge na pia mwanachama wa Baraza la Wataalamu wanamchagua Kiongozi Muadhamu. Aidha alikuwa Rais wa Iran katika duru mbili mfululizo na hatimaya mwaka 1989, baada ya kuaga dunia Imam Khomeini MA, alichaguliwa na Baraza la Wataalamu kuwa Kiongozi wa pili wa Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Aprili 1946, Syria ilipata uhuru kutoka kwa askari wa kigeni waliokuwa wakiitawala nchi hiyo. Syria na baadhi ya ardhi zinazoizunguka awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sham, na kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran, Ugiriki, Misri na Rome. Ardhi hiyo ilikuwa makao ya utawala wa Ugiriki na baada ya kukaliwa kwa mabavu na Misri, baadaye ilichukuliwa na utawala wa Othmaniya. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya kuporomoka utawala wa Othmaniya, Syria ilikoloniwa na Ufaransa. Kufikia Juni 1941, wakati wa vita vya pili vya dunia, askari wa Uingereza na Ufaransa waliikalia kwa mabavu nchi hiyo, hadi kufikia mwaka 1946 wakati ilipojipatia uhuru wake.

Bendera ya Syria

Miaka 41  iliyopita katika siku kama ya leo yaani 29 Farvardin mwaka 1358, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilimbai na kutangaza utiifu kwa Imam Khomeini MA, hayati Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kulifanyika gwaride mbali mbali kote Iran kutangza hadharani utiifu huo, hatua ambayo iliunga mkono na kukaribishwa na wananchi Waislamu wa Iran. Kwa msingio huo 29 Farvardin au tarehe 18 Aprili kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Siku ya Jeshi la Iran

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, mwafaka na tarehe 17 Aprili 2004, helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia gari lililokuwa limembeba Dokta Abdulaziz Rantisi, aliyekuwa mwanaharakati wa Palestina na kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, na kumuuwa shahidi. Dokta Rantisi alichaguliwa kuiongoza harakati ya Hamas baada ya kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin, mwasisi na kiongozi wa harakati hiyo. Rantisi alizaliwa mwaka 1947 katika mji wa Yafa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alihitimu elimu ya tiba kama daktari katika Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri.

Dokta Abdulaziz Rantisi akiwa pamoja na Sheikh Ahmad Yassin